24 Machi 2021 - 08:19
Mivutano baina ya Magharibi na nchi mbili za Russia na China yazidi kuwa mikubwa

Nchi mbili za Russia na China zimetaka kuitishwe kikao maalumu cha wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na kuongezeka sana mzozo baina ya nchi hizo mbili na Magharibi.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Russia na China ambazo uhusiano wao na nchi za Magharibi umeharibika sana katika miezi ya hivi karibuni, imetumia kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili kutoa mwito wa kuitishwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kitakachowashirikisha wanachama wa kudumu wa baraza hilo.

Katika tamko lao la pamoja, mawaziri wa mambo ya nje wa Russia na China wamesema, kuna haja ya kuitishwa kikao cha dharura cha wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na kuongezeka mizozo na mivutano katika uga wa kimataifa.

Kwa muda sasa Russia ilikuwa ikipigania peke yake kuitishwa kikao hicho lakini sasa hivi na kutokana na kushadidi mivutano baina ya China na nchi za Magharibi, imeamua kuishirikisha Beijing katika juhudi zake hio.

Katika tamko lao hilo la pamoja, Russia na China hazikuashiria hata kidogo Marekani lakini kwa mujibu wa ripoti za shirika la habari la Russia, Tass, baada ya maungumzo yake na waziri mwenzake wa China, Wang Yi; Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amesema, Moscow na Beijing haziridhishwi na vitendo vya Marekani.

Amesisitiza kuwa, Washington imeamua kufuata siasa za kipindi cha vita baridi ili kuangamiza mfumo wa sheria za kimataifa kupitia kuanzisha miungano ya kisiasa na kijeshi.

342/