20 Aprili 2021 - 11:59
Mwaka wa 75 wa Siku ya Uhuru wa Syria ya Idul-Jalaa

Mnamo karne ya 20, watu wa Syria walikoloniwa na Wafaransa kwa muda wa miaka 26. Wakoloni wa Kifaransa waliingia katika ardhi ya Syria mwaka 1920.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA:Na katika muda wa kuwepo kwao nchini humo, wakoloni hao walipora maliasili na wakahodhi na kuwanyang’anya Wasyria miliki zao na mazao yao ya kilimo. Hata hivyo tokea mwaka wa mwanzo wa kuingia wakoloni Wafaransa, wananchi wa Syria walianzisha mapambano na muqawama wa kukabiliana nao; na hatimaye tarehe 17 Aprili 1946 wakoloni  hao walisalimu amri mbele ya azma na irada ya watu wa Syria na kulazimika kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo. Kwa wananchi wa Syria, Aprili 17 ni Idul-Jalaa au Siku ya Uhuru, ambayo wanaisherehekea kila mwaka.

Baada ya kupita miaka 75 ya Idul-Jalaa, Syria ingali iko kwenye mapambano; lakini mapambano ya sasa, si dhidi ya ukoloni pekee bali yamechukua uwigo mpana zaidi. Leo wakoloni wamejiingiza tena ndani ya ardhi ya Syria kwa Marekani kuchukua nafasi ya Ufaransa. Wamarekani wamepiga kambi maeneo ya mashariki ya Syria na wanapora maliasili za nchi hiyo wakisaidiana na magaidi wa kundi la Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria SDF. Mbunge wa Syria Nidhal Mahna analizungumzia hivi suala hilo: “Kusema kweli, mapambano ya leo ni mwendelezo wa mapambano ya kupigania uhuru dhidi ya wakoloni. Mbinu na zana zimebadilika, lakini adui angali anainyemelea Syria na nchi zingine za eneo. Adui huyu ni wakoloni na utawala wa Kizayuni.”

Mbali na wakoloni, wananchi wa Syria wanalazimika pia kupambana na makundi ya kigaidi. Tangu mwaka 2011 hadi leo, wananchi wa Syria wako kwenye vita vya kupambana na ugaidi; magaidi ambao ni raia wa mataifa zaidi ya 80 na wanasaidiwa na kuungwa mkono na madola ya eneo hili la Asia Magharibi na nje yake. Magaidi hao waliingia Syria mwaka 2011 kwa lengo la kuuangusha utawala na kuigawanya vipande vipande nchi hiyo, lakini kwa msaada wa vikosi vya muqawama, wananchi wa Syria wamefanikiwa kuwashinda magaidi hao; ambapo mbali na kuuokoa mfumo wa utawala, wamefanikiwa pia kulinda umoja wa ardhi yote ya nchi yao.

Vikwazo pia ni jinamizi jengine la tatu ambalo wananchi wa Syria wamekuwa wakipambana nalo, hasa katika muongo huu wa karibuni. Wakoloni, ambao wameamua kutumia mbinu ya kuwasaidia na kuwaunga mkono magaidi ili kutoa pigo kwa Syria, sambamba na mbinu hiyo, wanatumia pia silaha ya vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Marekani kwa upande wake, inatumia sheria ya vikwazo ijulikanayo kama “Caeser”, na nchi za Ulaya zinatekeleza vikwazo vya aina tofauti ili kwa upande mmoja kuiwekea mbinyo serikali na wananchi wa Syria; na kwa upande mwingine kuendeleza uungaji mkono wao kwa makundi ya kigaidi. Kusema kweli magaidi na vikwazo ni silaha mbili muhimu ambazo wakoloni wa leo wanazitumia nchini Syria; hata hivyo muqawama na irada ya wananchi wa Syria imesambaratisha njama zao na wameshindwa kufikia malengo maovu waliyokusudia dhidi ya nchi hiyo.

Pamoja na yote hayo, suali muhimu la kujiuliza ni, kwa nini wananchi wa Syria, na baada ya kupita miaka 75, wangali wanapambana na wakoloni na makundi wanayoyaunga mkono?

Jibu la suali hili linapatikana kwenye hali ya jiopolitiki ya Syria na utambulisho wa nchi hiyo unaokinzana na malengo na maslahi ya wakoloni. Syria imepakana na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel); na kuuhami utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ni kipaumbele kikuu cha madola ya Magharibi, hususan Marekani. Kwa upande mwingine, katika utambulisho wake wa kisiasa, Syria ni mdau aliye karibu na mhimili wa muqawama akiwa mbali kabisa na mduara wa madola ya Magharibi. Kwa sababu hiyo, kuidhoofisha serikali kuu ya Syria kunaendana na maslahi ya utawala wa Kizayuni na ni sehemu ya vita vya mlingano wa nguvu kimataifa baina ya madola ya Mashariki na Magharibi. Na hiyo ndiyo sababu inayolifanya suala la kupambana na ukoloni liendelee kuwa sehemu ya utambulisho wa wananchi wa Syria…/

 342/