25 Aprili 2021 - 12:03
Rais Rouhani: Chanjo ya Covid-19 itatolewa kwa wananchi wote bila ya malipo

Rais Hassan Rouhani amesema, chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 itatolewa kwa wananchi wote bila ya malipo na amesisitiza kwamba, kuna ulazima wa kuwachukulia hatua watu wasiozingatia miiko ya marufuku zilizowekwa.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa sisitizo hilo leo katika kikao cha tume ya taifa ya kukabiliana na corona.

Huku akiashiria kwamba, kwa mujibu wa ripoti na takwimu, mikoa mingi nchini ingali ina idadi kubwa ya maambukizi; na takwimu za walioambukizwa, waliolazwa hospitalini na waliofariki dunia kwa maradhi ya Covid-19 zinaonyesha kuwa hali ingali ya kutia wasiwasi, Rais Rouhani amesema: "Hatuna njia nyingine yoyote isipokuwa kuhakikisha tunachukua hatua kali zaidi za udhibiti katika wiki hii au pengine wiki ijayo."

Rais wa Iran amesisitiza pia kuhusu ulazima wa kuundwa timu maalumu za usimamizi kwa ajili ya kuongeza hatua za tahadhari na kuzingatiwa kikamilifu misingi ya kiafya; na akasema, "vitengo vyote ambavyo kwa namna moja au nyingine vina jukumu la usimamizi, vinapaswa kuchukua hatua kali zaidi ili uzingatiaji wa miiko ya kiafya uwe mkubwa zaidi; kinyume na hivyo hatutaweza kulivuka wimbi hili."

Rais Rouhani ametanabahisha pia kuhusu hatari nyingine ya corona inayoikabili Iran ambayo amesema, ni ya kirusi cha corona cha India; na akafafanua kuwa kirusi cha India ni hatari zaidi kuliko kirusi cha Uingereza, Brazil, Afrika Kusini n.k, kwa hivyo kama kirusi hicho kitaingia nchini, Iran itakabiliwa na tatizo kubwa.

Kwa sababu hiyo amewataka wakuu wa mikoa ya Khorasan Razavi, Khorasan Jonubi, Sistan na Baluchistan na hata mikoa ya kusini ikiwemo ya Kerman na Hormuzgan wachukue hatua za tahadhari na kuelewa kwamba, wana kazi kubwa ya kuhakikisha kirusi hicho hatari hakiingii nchini.../

342/