Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Maandamano hayo yamefanyika mbele ya mahakama inayoshughulikia kesi ya afisa wa polisi, Derek Chauvin aliyepatikana na hatia ya kumuua George Floyd.
Washiriki wengi katika maandamano hayo walibeba picha za George Floyd na wahanga wengine wa mauaji yaliyofanywa na polisi wazungu wa Marekani. Wazungumzaji katika hadhara hiyo wametoa wito wa kukomeshwa dhulma na ubaguzi wa rangi uliokita mizizi katika utawala wa Marekani na kuutaka utawala huo "uondoe goti lake juu ya shingo za watu weusi".
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na shirika la habari la Associated Press yanaonesha kuwa, karibu watu 6 kati ya kila Wamarekani 10 wanaamini kuwa, ubaguzi wa rangi ni tatizo kubwa katika jamii ya Marekani.
Derek Chauvin, afisa mzungu wa polisi wa Marekani ambaye alimuua kikatili Mmarekani mwenye asili ya Afrika, George Floyd na kuzusha maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi dunia nzima hatimaye amepatikana na hatia katika mashitaka yote ya mauaji yaliyokuwa yakimuandama.
Afisa huyo mzungu alitiwa mbaroni tarehe 31 Mei mwaka jana kwa kosa la kumuua kikatili George Floyd katika mji wa Minneapolis huko Minnesota, magharibi mwa Marekani.
Mkanda wa video ulioenea sana katika mitandao ya kijamii, ulimuonesha afisa huyo mzungu wa polisi akimdidimiza kwa goti hadi kumuua Mmarekani huyo mwenye asili ya Afrika, mchana kweupe mbele ya kadamnasi ya watu, huku muhanga wa ukatili huo akilalamika hawezi kupumua hadi alipokata roho.
Mauaji hayo yalizusha maandamano ndani na nje ya Marekani ya kupinga ubaguzi wa rangi chini ya kaulimbiu "Black Lives Matter."
342/