Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Shirika la UNICEF limetangaza kuwa, tangu dunia ikumbwe na maambukizi ya kirusi cha corona hadi sasa shule katika nusu ya nchi za kanda ya Asia na Pacific zimefungwa kwa zaidi ya siku mia mbili. Huko Amerika ya Latini na ukanda wa Caribbean ambako shule zimefungwa kwa muda mrefu zaidi sasa shule zimefungwa kikamilifu au zinafundisha kwa masaa machache.
Huko mashariki na kusini mwa Afrika pia asilimia 40 ya watoto wote wenye umri wa kwenda shule wameshindwa kuanza masomo kutokana na janga la corona. Shirika la UNICEF limeongeza kuwa, utoaji mafunzo kwa njia ya mbali hautoshelezi hata kwa uchache theluthi moja ya wanafunzi duniani kote.
Msemaji wa UNICEF, James Elder amesema katika mkutano na waandishi wa habari huko Geneva kwamba, utumiaji mabavu, hofu na kutengwa vimechukua nafasi ya elimu, usalama, lishe na kujichanganya kwa marafiki miongoni mwa watoto.
Ameongeza kuwa, ingawa nchi mbalimbali duniani zimebakia njia panda baina ya kutekeleza hatua kali za protokali za afya za kuzuia maambukizi ya corona au kupunguza na kuondoa vizuizi vya kukabiliana na janga hilo, lakini kufungwa shule katika maeneo mbalimbali duniani kunapasa kuwa suala la mwisho katika kampeni za kuzuia janga la corona, na kwamba kufunguliwa shule kunapasa kupewa kipaumbele katika harakati za kuondolewa vizuizi vya kukabiliana na maambukizi ya corona.
342/