12 Agosti 2021 - 12:48
Wananchi wa Zambia wapiga kura kumchagua Rais

Maelfu ya wananchi waliokamilisha masharti wa Zambia wakiongozwa na Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo leo wamepiga kura katika uchaguzi wa rais unaofuatiliwa kwa karibu katika nchi hiyo ya kusini mwa bara la Afrika.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Lungu ambaye anagombea ili kuiongoza nchi hiyo kwa muhula mwingine anachuana vikali na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa leo, Hakainde Hichilema mwenye umri wa miaka 59. Uchaguzi wa leo wa rais huko Zambia unawashirikisha jumla ya wagombea 16. 

Edgar Lungu amewaambia waandishi wa habari mara baada ya kupiga kuwa mapema leo kwamba "Tuwaache wananchi waje wapige kura na kisha warejee nyumbani wasubiri matokeo kwa utulivu na amani." Amesema amewasikia baadhi ya wanasiasa wakiwataka wananchi kusubiri matokeo katika vituo vya kupiga kura jambo ambalo amesisitiza kuwa litaibua ghasia.

Lungu aliingia madarakani Zambia mwaka 2015 baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi mdogo uliogubikwa na malalamiko wa kukamilisha muhula wa urais wa mwendazake Michael Sata ambaye aliaga dunia akiwa madarakani. Edgar Lungu pia alichaguliwa kuwa Rais wa Zambia kuhudumu muhula wa miaka mitano kamili katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2016, ingawa mpinzani wake mkuu Hakainde Hichilema alipinga matokeo akisema kuwa yaligubigwa na wizi wa kura. Hii ni mara ya sita kwa mpinzani Hichilema kugombea kiti cha urais Zambia.  

Weledi wa mambo wanasema kuwa, matokeo ya uchaguzi wa rais wenye mchuano mkali wa Allhamisi hii kati ya mahasimu hao wawili wa kisiasa nchini Zambia yataweka wazi ramani ya uwekezaji katika nchi hiyo tajiri kwa madini ya shaba; ambako watu zaidi ya nusu ya jamii yote ya nchi hiyo wanaishi katika hali ya umaskini. Zambia ina jumla ya watu milioni 17.

342/