Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kanali Mamady Doumbouya, Mkuu wa Kikosi Maalumu cha Jeshi la Guinea anayeongoza kundi la wanajeshi waliofanya mapinduzi amesema katika hutuba yake kwenye televisheni ya taifa kwamba amevunja serikali na kusitisha katiba ya nchi na kwamba atafanya marekebisho ya katiba.
Mapinduzi ya Guinea yamefanywa na kikosi maalumu kilichoasisiwa mwaka 2018, na Kanali Mamady Doumbouya aliyeongoza mapinduzi hayo alikuwa askari katika kikosi cha jeshi la Ufaransa nje ya nchi.
Mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea Conakry yamekabiliwa na upinzani mkali wa jamii ya kimataifa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani kuchukuliwa madaraka kwa mtutu wa bunduki nchini humo na ametoa wito wa kuachiliwa huru mara moja Rais Alpha Conde. Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, na Mkuu wa tume ya AU Moussa Faki wameitisha mkutano wa dharura wa taasisi za umoja huo kuhusu usalama na amani ili kutathmini hali ya mambo nchini Guinea na kuchukua hatua zinazofaa. Taarifa ya pamoja ya viongozi hao wawil imesema: AU inalaani kitendo cha wanajeshi hao cha kutwaa madaraka nchini Guinea na inatoa wito wa kuachiwa huru mara moja Rais Alpha Conde.
Mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea yamefanyika baada ya rais wa nchi hiyo kubadili katiba ambayo imemruhusu kugombea kiti cha rais kwa mara ya tatu mfululizo. Awali katiba ya Guinea haikuwa ikimruhusu kuongoza nchi kwa zaidi ya vipindi viwili. Awamu ya pili ya Konde ilimalizika Disemba mwaka jana wa 2020. Hatua ya Rais Conde ilizusha malalamiko makubwa ndani na nje ya nchi hiyo.
Mbali na hayo serikali ya Alpha Conde pia haikuwa na mafanikio katika masuala ya uchumi. Conde ambaye ameiongoza nchi hiyo tangu Disemba mwaka 2010, amekuwa akisolewa sana kutokana na kutoheshimu sheria na mipango yake isiyofaa ya kiuchumi. Guinea inahesabiwa kuwa moja kati ya nchi maskini zaidi duniani licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa madini. Matatizo ya sekta ya afya kama maambukizi ya Ebola katika miaka iliyopita, ukosefu wa miundombinu muhimu kama ya huduma za maji na umeme, ufisadi na ubadhirifu mkubwa wa mali ya umma na kadhalika vilizidisha upinzani wa wananchi na migogoro ya kijamii nchini Guinea. Takwimu zinaonesha kuwa, nusu ya watu wa Guinea wanaishi chini ya mstari wa umaskini na asilimia kubwa ya watu nchini humo hawana huduma za maji na umeme.
Akiashiria hali hiyo mbaya ya Guinea, kiongoi wa mapinduzi ya kijeshi Kanali Mamady Doumbouya amesema: Umaskini mkubwa umekilazimisha kikosi chake kuiondoa madarakani serikali ya Conde na kuongeza kuwa: Miundombinu mibovu kama barabara na hospitali zisizofa inawafanya Waguinea kuamka baada ya miongo kadhaa ya uhuru wa nchi hiyo.
Baadhi ya duru zinadokeza kuwa, mivutano baina ya Rais Alpha Conde na Kanali Mamady Doumbouya ilipamba moto baada ya kutolewa pendekeo la kupunguzwa mishahara ya baadhi ya wanajeshi. Vilevile katika wiki za karibuni serikali ya Conakry imezidisha sana ushuru kwa ajili ya kupata fedha za kujaza nakisi ya bajeti. Pia imepandisha juu bei ya mafuta ya petroli kwa asilima 20, suala ambalo limeibua malalamiko ya wananchi.
Ingawa hali ya Guinea kwa sasa inaripotiwa kuwa ni shwari lakini hali ya kisiasa ya nchi hiyo inaendelea kulegalega. Vinara wa mapinduzi ya kijeshi ya Guinea wameahidi kurejesha amani na kuboresha maisha ya wananchi ingawa bado wanalaumiwa kwa kukanyaga demokrasia na utawala wa sheria. Hii ni pamoja na kuwa, uzoefu unaonesha kwamba mara nyingi ahadi zinazotolewa na wafanyamapinduzi huwa hazitekelezwi, na kinume chake, mapinduzi kama haya ya kijeshi hutayarisha uwanja wa kuingilia kati madola ya kigeni kama Ufaransa katika masuala ya ndani ya nchi kama Guinea Conakry.
342/