22 Oktoba 2021 - 17:31
IMF: Uchumi wa Afrika utaimarika mwaka huu

Uchumi wa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara unatarajiwa kuimarika mwaka huu 2021 baada ya kuporomoka mwaka uliotangulia wa 2020 kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya mtazamo wa uchumi katika ukanda huo, ripoti iliyotolewa Alhamisi na Shirika la Fedha Duniani, IMF ikisema kuwa uchumi utakua kwa asilimia 3.7 mwaka huu wa 2021 na asilimia 3.8 mwaka ujao wa 2022.

IMF inasema inakaribisha kwa dhati ukuaji huo unaochochewa na mazingira bora ya uchumi nje ya ukanda huo ikiwemo ongezeko kubwa la biashara na bei za bidhaa.

Mkuu wa Idara ya Afrika katika IMF Abebe Aemro Sellasie akizungumzia makadirio hayo amesema “ukuaji unatokana pia na kuimarika kwa mavuno na ongezeko la uzalishaji katika sekta ya kilimo kwenye nchi kadhaa.”

IMF hata hivyo imetahadharisha kuwa, ukanda huo wa Afrika uko katika mwelekeo tofauti usio wa kuridhisha katika kujikwamua ikilinganishwa na maeneo mengine, na kwamba tofauti hiyo kimataifa ambayo inatarajiwa kuwepo kwa muda, imechangiwa na kasi ndogo ya bara hilo katika kuendesha kampeni za chanjo dhidi ya Corona.

Kasi ndogo ya chanjo katika nchi nyingi za Afrika imesababishwa na mambo kadhaa ikiwemo ukosefu wa chanjo unaotokana na baadhi ya nchi kuhodhi kiwango kikubwa cha chanjo huku nyingine zikiwa hazina kabisa. Hali kadhalika baadhi ya nchi kuweka vikwazo kwa kampuni za chanjo kutouza nje ya nchi chanjo hizo za Corona na wengine wakisaka chanjo ya tatu, hali inayoweza kukwamisha usambazaji wa chanjo kwa nchi ambazo bado hazijafikia wananchi wake wote.

Aidha IMF imeonya kuwa ukwamukaji wa uchumi katika ukanda wa Afrika kusini mwa jangwa la Sahara bado uko tete na unategemea pia mtazamo wa uchumi wa dunia ikiwemo mazingira magumu ya kifedha duniani.


/