30 Desemba 2021 - 10:59
HAMAS: Njama mpya za Israel huko Golan ni hujuma dhidi ya Waarabu

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesema mpango mpya wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Miinuko ya Golan ya Syria ni hujuma ya moja kwa moja dhidi ya Waarabu wote.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Hazem Qassem, Msemaji wa HAMAS alisema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, njama hizo mpya za utawala haramu wa Israel za kuongeza maradufu ujenzi wa vitongoji hivyo haramu ni chokochoko dhidi ya haki na ardhi za jamii yote ya Waarabu, na vile vile ni muendelezo wa uvamizi wa utawala huo khabithi dhidi ya Wapalestina.

Wakati huohuo, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imelaani vikali mpango huo ulioidhinishwa na utawala wa Kizayuni, wa kujenga nyumba mpya 7,300 katika eneo hilo la Syria linalokaliwa kwa mabavu.

Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Arab League amesisitiza kuwa, hatua zinazochukuliwa na utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya kubadili utambulisho na hali ya kisheria ya eneo la Golan la Syria ni batili na zinakiuka kanuni na sheria za kimataifa. 

Mapema mwezi huu, Umoja wa Mataifa ulipasisha azimio linalolaani na kubatilisha hatua zote za Israel katika eneo la Syria la Golan linalokaliwa kwa mabavu na utawala huo na kuutaka utawala wa Kizayuni ukomeshe hatua zote zinazokiuka sheria za kimataifa.

Kabla ya hapo pia, Umoja wa Mataifa ulipasisha azimio lililoitaka Israel kuondoka kikamilifu eneo la Golan la Syria na kurejea katika mpaka wa tarehe 4 Juni mwaka 1967. 


342/