Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Osinbajo amesema hayo wakati alipoonana na waziri wa masuala ya Afrika wa Uingereza, Vicky Ford na kuongeza kuwa, wimbi la mapinduzi ya kijeshi hasa katika nchi za magharibi mwa Afrika limeongezeka sana. Amesema, anahisi kuna umuhimu wa kufikiria njia za kuzuia kutokea mapinduzi hayo kupitia kuwa na ushirikiano wa karibu baina ya nchi za eneo hilo na pia na mataifa na taasisi za nje.
Amesema, moja ya mambo nyeti na muhimu sana ambayo yamejadiliwa katika vika mbalimbali vya ECOWAS ni kushirikiana na mataifa mengine duniani, taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na baadhi ya taasisi za fedha za kimataifa ili kuhakikisha kuwa vikwazo vinavyowekwa dhidi ya wanajeshi wanaofanya mapinduzi vinakuwa na nguvu za kweli za kukwamisha mapinduzi hayo.
Eneo la magharibi mwa Afrika limekumbwa na wimbi la mapinduzi ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni. Mwaka 2020 yalitokea mapinduzi mengine ya kijeshi nchini Mali. Mwezi Septemba 2021 mapinduzi mengine ya kijeshi yalitokea Guinea. Mapinduzi mengine ya kijeshi ni ya mwezi uliopita wa Januari 2022 nchini Burkina Faso.
Wiki moja tu nyuma wanajeshi wenye silaha walijaribu kumpindua Rais wa Guinea-Bissau kwa kutumia mtutu wa bunduki. Mapigano yaliendelea kwa masaa kabla ya jaribio hilo kuzimwa. ECOWAS muda wote imekuwa ikilaani mapinduzi hayo na kuweka vikwazo dhidi ya wanajeshi wanaofanya mapinduzi lakini vikwazo hivyo vimeshindwa kuvunja nguvu tawala za kijeshi zilizotwaa madaraka kinyume na demokrasia.
342/