13 Aprili 2022 - 16:21
Athari za vita vya Ukraine Asia Magharibi; Israeli katika kilele cha waliofaidika na vita hivyo

Kwa kawaida, vita vyote huwa na gharama na hasara isipokuwa kwa wamiliki wa sekta ya silaha ambao wamewekeza fedha nyingi na wanasubiri vita na mvutano ili wauze silaha na bidhaa zao.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Wamiliki wa viwanda vya zana za kijeshi pia hutumia vita kufanyia majaribio na kuonyesha silaha zao mpya, wakiwaringishia au kutunisha misuli mbele ya wapinzani na maadui zao. Kwa upande mwingine, vita husababisha hasara na uharibifu mkubwa kwa watu wengi, hasa raia na watu wa kawaida, hata katika maeneo ya mbali zaidi ya mazingira ya vita, na huenda hata vikagharimu maisha ya mamilioni ya watu kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na kupanda kwa gharama za bidhaa na huduma mbalimbali. Kwa sasa madhara ya vita vya Ukraine yanaonekana duniani kote kutokana na kutegemeana kwa nchi mbalimbali katika mfumo wa dunia wa kiuchumi, na huenda isiwezekane kupata sehemu ambayo imesalimika kutokana na madhara na matokeo mabaya ya vita hivyo.

Katika eneo la Asia Magharibi, vita vya Ukraine vimekuwa fursa kwa madola machache, lakini tishio kwa serikali na mataifa mengi zaidi.

Utawala haramu wa Israel na Saudi Arabia ni miongoni mwa tawala chache zilizonufaika na vita vya Ukraine, na kuna uwezekano kwamba zimekuwa na mchango katika kuibuka vita hivyo, hasa kutoka upande wa Israel na mafia wake wenye ushawishi kwa pande zote mbili zinazozozana katika mgogoro huo.

Vita vya Ukraine vimeipatia Israel fursa ya kuhamisha idadi kubwa ya Wayahudi wa Ukraine na wa maeneo mengine yanayokumbwa na machafuko na kuwapeleka Palestina inayoikaliwa kwa mabavu ambako inawapa makazi katika vitongoji haramu vilivyojengwa kwenye ardhi ya iliyoghusubiwa ya Palestina. Utawala wa Kizayuni unaohisi hatari na kutishwa na ongezeko la idadi ya watu wa Palestina na athari zake katika kubadilisha mlingano wa kidemografia, unaliona suala la hata kumhamisha mhajiri mmoja wa Kiyahudi na kumpeleka katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kuwa ni fursa yenye umuhimu, na kwa kawaida chama kinachotawala huliorodhesha suala hilo katika rekodi ya mafanikio yake. Vita vya Ukraine pia vimezua vikwazo vipya katika mazungumzo ya nyuklia ya Iran na uwezekano wa serikali ya Biden kurejea katika mapatano ya JCPOA, jambo ambalo utawala wa Kizayuni wa Israel umetumia nguvu zake zote kwa ajili ya kulifanikisha. Aidha utawala wa Kizayuni unadhani kuwa kutokana na changamoto zitakazosababishwa na vita vya Ukraine kwa Russia, utapata ushawishi zaidi katika maeneo kama vile Russia au katika mafaili yanayoihusu nchi hiyo.

Kwa upande wa Saudi Arabia, kama ilivyo kwa Israeli, vita vya Ukraine vimekuwa na fursa nyingi, kwa uchache hadi sasa, kuliko vitisho vyake. Kutokana na athari zake katika ongezeko la bei ya nishati duniani hususan katika nchi zinazotumia mafuta kwa wingi za Magharibi zikiwemo Marekani na Ulaya, vita hivyo vimeiongezea Saudi Arabia nguvu ya kufanya mazungumzo dhidi ya nchi hizo zilizopunguza uhusiano wao na Riyadh baada ya kubainika kuhusika moja kwa moja mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman katika mauaji ya Jamal Khashoggi. Kwa sababu hiyo tumeshuhudia kwamba baada ya kuanza vita vya Ukraine, Uturuki imetupilia mbali kesi hiyo na kukabidhi faili lake kwa Saudi Arabia yenyewe inayoshutumiwa kwa mauaji hayo!

Saudi Arabia pia imewasilisha matakwa yake kwa nchi za Magharibi zilizotaka kuongezwa kiwango cha uzalishaji wa mafuta kutokana na kupungua bidhaa hiyo duniani kwa sababu ya vita vya Ukraine; jambo ambalo linaweza kuzidisha vita nchini Yemen. Wakati huo huo, kutokana na ongezeko la mapato yake yanayotokana na mafuta, Saudi Arabia itaweza kujiunga na miradi ya kupindua tawala na serikali za nchi mbalimbali za eneo la Magharibi mwa Asia ikishirikiana na Israel, na jambo hili limedhihirika katika kuondolewa madarakani serikali ya Imran Khan nchini Pakistan ambaye nafasi yake imechukuliwa na mtu aliye karibu na Saudi Arabia.

Katika upande mwingine vita vya Ukraine vimekuwa na athari mbaya kwa nchi na mataifa mengi ya Asia Magharibi na Afrika, hasa yale ambayo hayana mapato ya mafuta au yanasumbuliwa na vikwazo vya miaka mingi vya Marekani na washirika wake kama vile Russia. Kupanda kwa bei za bidhaa za chakula, hasa mkate na nafaka zinazozalishwa na nchi za Ukraine na Russia, sio tu kwamba kumeongeza gharama za maisha, bali pia kumezidisha uwezekano wa kutokea vuguvugu la maandamano katika baadhi ya nchi kama lile linalojulikana kama Arab Spring. Jambo hilo yumkini likawa fursa mpya kwa Israeli ya kuziburuta nchi zingine za Kiarabu kwenye mzingo wa mapatano na kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo.

Kwa ujumla, tunaweza kusema kwamba vita vya Ukraine vimekuwa na faida kwa idadi ndogo sana ya nchi na madola hususan utawala haramu wa Israel na mafia wa Mayahudi. Ama kwa aghlabu ya nchi na mataifa ya dunia, vita vya Ukraine vimekuwa balaa na tishio kubwa ambalo hapana budi kushughulikiwa haraka iwezekanavyo ili pamoja na kukomesha balaa hilo, walimwengu waweze kukabiliana na madola na tawala zinazotumia vibaya vita na machafuko kwa ajili ya kutimiza malengo yao ya kishetani. 

342/