Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Muhammad bin Salman katika miaka mitano ya karibuni amewatia nguvuni na kuwakandamiza jamaa wengi wa aila hiyo ya kifalme na wa serikali ya Saudia ili kujisafishia njia ya kushika hatamu za ufalme wa nchi hiyo baada ya baba yake. Shakhsia wengi ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani, idara za usalama, taasisi za utendaii, viongozi wa dini, wanaharakati wa taasisi za kiraia na wa vyombo vya mahakama ni kati ya wanawafalme waliotiwa nguvuni na utawala wa Saudia chini ya uongozi wa mrithi wa kiti cha ufalme Muhammad bin Salman; ambapo kilele cha kamata kamata hiyo kilikuwa mwezi Novemba mwaka 2017. Sababu kuu ya kutiwa nguvuni watu hao imetajwa kuwa ni kupambana na ufisadi ikiwemo kupambana na fedha zisizo salama, vitendo vya rushwa, vitendo vya kughushi na ubadhirifu.
Ufisadi umeongezeka pakubwa katika muundo wa utawala nchini Saudi Arabia. Suala hili bila shaka linatokana na mfumo wa kisiasa wa Saudia ambao unaendeshwa kifamilia. Madaraka ya kuendesha nchi yanagawiwa watu katika ukoo wa Aal Saud huku wananchi wakiachwa bila ya kuwa na nafasi yoyote katika muundo wa madaraka. Muundo kama huo bila shaka ni chanzo cha kuenea ufisadi nchini. Katika uwanja huo, viongozi wa Saudia mwezi uliopita waliwatia nguvuni maafisa wa serikali 143 kutoka wizara sita zikiwemo Wizara za Ulinzi na ya Mambo ya Ndani; na watu 544 ni kati ya watuhumiwa waliochunguzwa mwezi Februari mwaka huu katika kesi hizo za ufisadi.
Nukta nyingine ni kuwa, vita dhidi ya ufisadi vinafuatiliwa pakubwa nchini Saudia tangu Muhammad bin Salman akalie kiti cha mrithi wa kiti cha ufalme mwaka 2017. Katika uwanja huo, Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Ufisadi ya Saudia hivi karibuni ilitangaza kuwa mwaka jana wa 2021 ilianza kutekeleza majukumu yake ya kupambana na ufisadi na tayari imeshasimamia kesi 34,825 na kuwachunguza watuhumiwa 7,648 wanaokabiliwa na kesi za masuala ya kiidara, jinai mbalimbali na ufisadi wa fedha. Aidha kupitia uchunguzi huo, watuhumiwa 2,460 wametiwa nguvuni huko Saudia ili kukamilisha kile kilichotajwa kuwa marhala ya kawaida; na kesi zao tayari zimefikishwa mahakamani. Hadi sasa mamia ya watu wakiwemo wanawafalme, maafisa polisi na maafisa wa taasisi za serikali wamehukumiwa kutumikia vifungo jela na kulipa faini.
Suala jingine muhimu ni kuwa, Utawala wa Aal Saud unatekeleza kamatakamata na kuwatia watu nguvuni bila ya kuwaleza tuhuma zinazowakabili na katika mazingira yasiyo wazi. Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa sheria, mtuhumiwa anapasa kuelezwa sababu ya kutiwa nguvuni pamoja na kuwa na uelewa sahihi wa mashtaka yanayomkabili. Kukuza propaganda kuhusu vita dhidi ya ufisadi katika vyombo vya habari vya Saudia ni fursa ambayo amekuwa akiitumia mrithi huyo wa kiti cha ufalme kwa maslahi yake ya kibinafsi.
342/