Shirika la habari la FARS limemnukuu Brigedia Jenerali Mohammad-Reza Gharaei Ashtiani akisema hayo jana wakati alipoonana na Jenerali Zaheer Ahmad Babar Sidhu, Kamanda wa Jeshi la Anga la Pakistan na kuongeza kuwa, hali katika matukio ya kimataifa hivi sasa ni tata sana. Amesema, Marekani waliiikalia kwa mabavu Afghanistan kwa muda wa miaka 20 lakini hatimaye wamelazika kukimbia kwa madhila nchini humo.
Aidha Brigedia Jenerali Ashtiani ameelezea kusikitishwa kwake na maafa makubwa yaliyosababishwa na mafuriko ya hivi karibuni huko Pakistan na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan zina mambo mengi ya kuzikutanisha pamoja kuanzia ya kihistoria hadi ya kiutamaduni, kijamii na kidini.
Pia amesema, Iran na Pakistan ziko kwenye maeneo muhimu kijiografia na uwepo wao kwenye maeneo hayo una taathira katika matukio ya kieneo na kimataifa hasa katika Ulimwengu wa Kiislamu na kwamba muda wote Pakistan imekuwa na nafasi ya kipekee katika siasa za mambo ya nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa upande wake, Jenerali Zaheer Ahmad Babar Sidhu, Kamanda wa Jeshi la Anga la Pakistan ambaye ametembelea Iran kwa mwaliko rasmi amesema, kuna udharura wa kuimarishwa uhusiano wa kijeshi na kiulinzi baina ya nchi hizi mbili ndugu za Kiislamu hasa kutokana na matukio ya hivi karibuni yaliyotokea duniani na katika ukanda huu mzima yakiwemo matukio ya Afghanistan.
342/