5 Septemba 2022 - 16:09
Mcheza karate wa Kuwait akataa kucheza na Muisraeli mjini Baku

Mpiganaji wa karate wa Kuwait Mohammad al-Otaibi amejiondoa katika mashindano ya 2022 ya Ligi Kuu ya Karate 1 katika mji mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan, Baku, ili kuepuka kukabiliana na mwakilishi wa utawala haramu wa Israel.

Al-Otaibi amechukua hatua hiyo kutokana uungaji mkono wake kwa kadhia ya ukombozi wa ardhi za Palestina zinazokoliniwa na utawala dhalimu wa Israel na pia kama ishara ya kupinga hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo.

Otaibi alipangwa kushiriki katika kitengo cha kilo 60 cha wanaume cha mashindano hayo ya kimataifa. Hata hivyo, alijiondoa katika mashindano hayo mara tu alipogundua kuwa amepangiwa kumenyana na mwakilishi wa utawala wa Israel, Ronen Gehtbarg.

Haya yanajiri huku wanariadha kutoka nchi za Kiislamu wakikataa mara kwa mara kushindana dhidi ya wakilishi wa Israel katika mashindano makubwa ya kimataifa kupinga jinai za utawala huo haramu ambao unaendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Hii si mara ya kwanza kwa mwanamichezo wa Kuwait kukataa kucheza na Muisraeli. Mwezi Aprili mchezaji wa  vitara (fencing) kutoka Kuwait, Mohamed Al Fadli alijiondoa katika mashindano ya Ubingwa wa Kimataifa wa Vitara katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ili kujizuia kukutana na Muisraeli. Fadli pia alijiondoa katika mashindano ya kimataifa katika mji mkuu wa Uholanzi, Amsterdam, mnamo Septemba 2019, baada ya droo hiyo kumweka katika kundi linaloshindana na mchezaji wa Israeli.

342/