23 Septemba 2022 - 18:13
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran: "Adui anachochea machafuko;" maandamano ya kulaani fujo yafanyika kote nchini

Wananchi wa Tehran na wa maeneo mengine yote ya Iran leo baada ya Sala za Ijumaa, wameshiriki kwa wingi katika maandamano makubwa ya kulaani magenge ya wanaofanya fujo, kuchoma mali za uma, kuvunjia heshima matukufu ya kidini na kijamii ya wananchi wa Iran.

Wakati wananchi wengi wa Iran wameguswa na kusikitishwa na kifo cha Mahsa Amini na hivi sasa wanasubiri kutangazwa rasmi matokeo ya uchunguzi wa sababu ya kifo chake, imefanyika mikusanyiko ya malalamiko na upinzani katika baadhi ya miji ukiwemo wa Tehran ambayo imesababisha uharibifu wa mali za umma.

Ijapokuwa idadi ya wanaofanya fujo ni ndogo na licha ya kwamba wafanya fujo hao ni wale wale wenye historia ya kushiriki katika maandamano ya fujo kila yanapotokea, lakini vyombo vya habari vya maadui wa taifa la Iran vinakuza kupindukia matukio hayo na kudai kuwa wahalifu hao wanawakilisha wananchi wa Iran.

Kabla ya kuanza maandamano ya kulaani fujo hizo hapa Tehran, Sayyid Ahmad Khatami alikuwa amesema kwenye khutba za Sala ya Ijumaa kwamba, kufariki dunia mwananchi yoyote ni jambo la kusikitisha na inabidi kuipa mkono wa pole familia ya marehemu. 

Amesema, viongozi wote wa ngazi za juu humu nchini wamechukua hatua za kufuatilia kifo hicho na hilo linaonesha ni kiasi gani viongozi hao wana huruma na wananchi wao. Ameongeza kuwa, kwa muda mrefu adui wa taifa la Iran alikuwa anatafuta fursa ya kuchochea machafuko lakini alikuwa ameshindwa. Amesisitiza kuwa, kisingizio kilichotumiwa na wafanya fujo hao ni cha ajabu sana hasa kutokana na kuwa viongozi wakuu humu nchini wako mstari wa mbele kushughulikia kifo cha Mahsa Amini na hakuna sababu yoyote ya kufanya vurugu.

Baada ya khutba hiyoi, wananchi wanamapinduzi wa Tehran na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wamefanya maandamano hayo makubwa kote nchini ili kuwaonesha maadui kuwa wahalifu hao hawawakilishi hata asilimia ndogo tu ya wananchi wa taifa hili la Kiislamu.

Aidha leo na kabla ya Sala ya Ijumaa hapa Tehran, kumefanyika kumbukumbu ya kifo cha Mtume Muhammad SAW na kuuawa shahidi Imam Hasan al Mujtaba AS na Imam Ridha AS na wametangaza hasira zao kwa wahalifu wanaoharibu mali za umma na kuvunjia heshima matukufu ya kidini na kijamii ya wananchi wa Iran.

Katika matangazo ya vyombo vya habari vya uchocheaji ghasia na hatua dhidi ya Iran, chombo cha habari cha utawala wa Saudi Arabia cha Iran International na BBC Farsi ya serikali ya Uingereza, ndizo zinazoendesha zaidi kampeni ya kuchochea machafuko hayo.

Ifahamike kuwa tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mnamo mwaka 1979, zaidi ya watu 17,000 wakiwemo raia na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameuawa shahdi katika hujuma na mashambulio ya gengo la Munafikina (MKO) na makundi mengine ya kigaidi.


342/