17 Oktoba 2022 - 19:35
Papa Francis akosoa utendaji wa Umoja wa Mataifa

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amekosoa utendaji dhaifu wa Umoja wa Mataifa katika masuala mbalimbali.

Gazeti la La Stampa la Italia limeripoti kuwa, Papa Francis ametoa wito wa kufanyika marekebisho katika Umoja wa Mataifa hususan Baraza la Usalama la umoja huo na kusema: Janga la COVID-19 na vita vya Ukraine vimefichua udhaifu wa Umoja wa Mataifa. 

Likitegemea matamshi ya Papa Francis katika kitabu chake kipya kilichopewa jina la: “I Ask You in the Name of God: Ten Prayers for a Future of Hope", gazeti la La Stampa limeandika kuwa, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki ameukosoa Umoja wa Mataifa kuwa haufai tena kwa ajili ya kukabiliana na hali halisi iliyopo hivi sasa na ameshutumu vita na umiliki wa silaha za nyuklia kuwa ni utovu wa maadili, akisema mataifa yasiyo na dhamira yanaendelea kuzalisha silaha hizo.

Amelihimiza Baraza la Usalama kuwa "athirifu na lenye ufanisi zaidi katika kutatua migogoro" na kuutaka Umoja wa Mataifa kwa ujumla kutekeleza "mageuzi ya kimsingi" ambayo yatasaidia katika "kuhudumia familia ya mwanaadamu". 

Katika kitabu hicho, Papa Francis amesema kwamba, hatua za Umoja wa Mataifa haziwezi kujibu na kuwa suluhisho la hali halisi na mpya ya kimataifa.

342/