Abdullah Abdullah amekutana na Balozi wa Iran mjini Kabul, Afghanistan na kushukuru misaada ya kibinadamu inayotolewa na Jamhuri ya Kiislamu kwa wananchi wa Afghanistan na hatua ya Iran ya kuwapokea mamilioni ya wakimbizi wa Kiafghani na kueleza kuwa wananchi hao siku zote wanashukuru misaada wanayopata kutoka Iran.
Katika mazungumzo hayo, Bahadur Aminian Balozi wa Iran nchini Afghanistan pia ameashiria uhusiano mkongwe na wa kihistoria kati ya nchi mbili na kusema: "Iran iko pamoja na wananchi wa Afghanistan kama ilivyokuwa huko nyuma na itawasaidia raia hao kadiri inavyoweza."
Abdullah amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran huko Kabul katika fremu ya siasa za Tehran kwa ajili ya kudumisha mawasiliano na mazungumzo na makabila tofauti huko Afghanistan kwa lengo la kusaidia kurejesha amani na utulivu nchini humo na kuandaa mazingira ya kuundwa serikali shirikishi itakayoimarisha mshikamano ndani ya nchi hiyo.
Aidha katika sera zake mkabala wa Afghanistan tangu kundi la Taliban lishike tena hatamu za uongozi huko Afghanistan mwezi Agosti mwaka jana hadi sasa Iran imekuwa ikisisitiza juu ya ulazima wa kuundwa serikali shirikishi nchini humo kwa kuyashirikisha makabila na makundi yote ya kisiasa ya nchi hiyo.
Licha ya kwamba katika upande wa kisiasa, Iran inaamini kuwa, kuundwa serikali jumuishi huko Afghanistan ni moja ya njia za kurejesha amani nchini humo; katika muda wa zaidi ya mwaka mmoja uliopita na hivi sasa ambapo kundi la Taliban limeingia tena madarakni, Iran kama ilivyokuwa huko nyuma imeendelea kutuma misaada mikubwa kwa watu wa majimbo mbalimbali ya Afghanistan.
Katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja uliopita Afganistan imekumbwa na matatizo makubwa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na Marekani kuzuia fedha za Benki Kuu ya nchi hiyo nje ya nchi, kupungua pakubwa thamani ya sarafu ya nchi hiyo na misaada ya kifedha na isiyo ya kifedha kutoka jamii ya kimataifa na pia kuongezeka sana kwa gharama za maisha.
Ndio maana taasisi na mashirika mbalimbali ya kimataifa yakatahadharisha mara kadhaa kuhusu kutokea maafa makubwa ya njaa miongoni mwa mamilioni ya wananchi wa Afghanistan na kuitolea wito jamii ya kimataifa kuzingatia hali nyeti ya mambo nchini humo.
Wakati huo huo pamoja na Afghanistan kukatiwa au kupunguziwa pakubwa misaada ya kimataifa kwa kisingizio cha kuingia madarakani kundi la wanamgambo wa Taliban, lakini Iran kama ilivyofanya katika miongo iliyopita imeendelea kutoa misaada kwa watu wa Afghanistan ambao kwa miaka mtawalia wamekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe au kukaliwa kwa mabavu na nchi ajinabi.
Licha ya kuingia madarakani huko Afghanistan tawala mbalimbali katika miongo kadhaa iliyopita, lakini Iran siku zote imekuwa bega kwa bega na kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo. Wananchi wa Afghanistan wamepongeza na kusifia sera za Iran kutokana na kitendo chake cha kutuma katika miaka ya karibuni misaada ya kibinadamu kwa ajili ya nchi hiyo inayojumuisha bidhaa mbalimbali za chakula, dawa za matibabu na vifaa tiba na hasa katika kipindi cha janga hatari la Uviko-19.
Bila shaka aina ya mienendo ya kibinadamu ya Iran kwa wananchi madhulumu wa Afghanistan na wakimbizi wa nchi hiyo, mbali na wananchi wa Afghanistan, imezipelekea pia taasisi za kieneo na kimataifa kusifia siasa za Tehran mkabala wa Afghanistan. Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa imepongeza katika ripoti yake kuhusu hali ya wakimbizi wa Kiafghani duniani kuhusu jitihada na hatua za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuwapokea karibu wakimbizi wa Kiafghani milioni 3.6 na kuitaja Iran kuwa nchi mfano na inayopasa kuigwa katika swala la kuwa nchi mwenyeji inayowapokea wakimbizi.
342/