14 Desemba 2022 - 21:06
Tathmini juu ya kikao cha Tehran cha "Mashirikiano Kamili ya Kimkakati kati ya Iran na China"

Kikao cha mpango wa "Mashirikiano Kamili ya Kimkakati baina ya Iran na China" kilianza jana Jumanne hapa mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Naibu Waziri Mkuu wa China.

Ajenda kuu ya kikao hicho ni kujadili njia za kuupa msukumo zaidi mchakato wa utekelezaji wa mpango huo kamili wa ushirikiano wa miaka 25 kati ya Iran na China. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Mohammad Mokhber na Naibu Waziri Mkuu wa China Hu Chunhua ndio wanaoongoza jumbe za nchi mbili katika kikao hicho.Tangu miaka kadhaa iliyopita, Iran na China zimepanua na kustawisha uhusiano wao katika ngazi tatu kuu za "kisiasa-kiuchumi", kiusalama-kiulinzi" na "kijiopolitiki-kistratejia"; na kusainiwa hati ya kimkakati ya miaka 25 inahesabiwa kuwa hatua muhimu katika kukamilisha mchakato huo. Mnamo mwezi Machi 2021, Iran na China zilitia saini hati ya Mpango Kamili wa Mashirikiano ya miaka 25, hatua inayotajwa kama harakati ya upeo wa juu zaidi katika uhusiano wa nchi mbili.

Hati hiyo ndio dira ya ushirikiano wa muda mrefu baina ya nchi mbili katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na China zina maslahi ya pamoja pia ya kistratejia na ya muda mrefu katika kukabailiana na kudhibiti sera za Marekani za kujichukulia hatua za upande mmoja; na ushirikiano huo wa Tehran na Beijing una taathira muhimu kwa matukio ya kikanda. Kuwemo katika ujumbe ulioandamana na Naibu Waziri Mkuu wa China katika safari yake ya Tehran wadau wa sekta za biashara na uchumi wakiwemo makumi ya wafanyabiashara wakubwa wa nchi hiyo ni ushahidi kwamba, kutokana na uelewa mzuri ilionao juu ya uwezo na fursa nyingi zilizopo Iran zikiwemo za sekta ya nishati, Beijing ina hamu ya dhati ya kutekeleza hati kamili ya ushirikiano wa miaka 25 na Iran.

Lakini pamoja na hayo, kitu kilichoongeza umuhimu wa safari ya ujumbe wa China hapa nchini ni kufanyika safari hiyo katika hali ambayo, mnamo siku ya Jumamosi na baada ya kumalizika kikao cha pamoja cha China na nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi kilichofanyika Riyadh, Saudi Arabia, pande hizo mbili zilitoa taarifa ya pamoja ambayo sehemu yake moja inasema: "tunaunga mkono jitihada zote zinazofanywa kwa njia ya amani na Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa ajili ya kupata suluhisho katika kadhia ya visiwa vitatu kupitia mazungumzo ya pande mbili na kwa kufuata vigezo vya kanuni za kimataifa na kulitatua suala hili kwa kuzingatia sheria za kimataifa".

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian alitoa jibu kwa taarifa hiyo katika ujumbe alioandika kwa Kichina kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema: "visiwa vitatu vya BuMousa, Tomb Ndogo na Tomb Kubwa katika Ghuba ya Uajemi ni sehemu isiyotenganika ya ardhi ya Iran; na itabaki daima kwenye ardhi yake ya asili. Iran haitafanya mapatano na nchi yoyote juu ya umuhimu wa kuheshimiwa umoja wa ardhi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran". 

Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian

Hatua ya hivi karibuni iliyochukuliwa na China ya kuungana kimsimamo na nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (GCC) ikiwemo Saudi Arabia imewafanya baadhi ya weledi wa mambo watafsiri kwamba Beijing imebadilisha sera zake kuhusiana na eneo hili, lakini Beijing yenyewe imelikana dai hilo kama alivyoeleza msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo Wang Wenbin ya kwamba: "nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi na Iran, zote ni marafiki wa China; si uhusiano wa China na Baraza la Ushirikiano wa Ghuuba ya Uajemi, wala uhusiano wa China na Iran ulio dhidi ya upande wowote wa tatu".

Wenbin vilevile amesema, Iran na China ni marafiki wa tangu na tangu na akaeleza kwamba nchi hizo mbili zimeamua kwa pamoja kuimarisha na kustawisha ushirikiano wao kamili wa kimkakati. China imeonyesha kuwa iko tayari kuongeza kiwango cha mawasiliano na mashauriano na Iran kwa ajili ya kupiga hatua zaidi katika uhusiano wa pande mbili. Ni wazi kwamba sababu za kiuchumi na kibiashara zinadhihirisha kwa uwazi zaidi jinsi Beijing inavyozipa umuhimu nchi za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi.


342/