9 Januari 2023 - 15:16
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran: Kitendo cha Jarida la Ufaransa ni mfano wa wazi wa matamshi ya chuki

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekitaja kitendo cha jarida la Ufaransa la Charlie Hebdo kuwa ni mfano wa wazi wa matamshi ya chuki na udhalilishaji wa thamani za wengine.

Naser Kan'ani Chafi amesema leo katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari hapa Tehran kuhusu kitendo cha jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo la kuwavunjia heshima wanazuoni wa kidini kwamba, kitendo cha jarida hilo la Kifaransa ni mfano wa wazi wa matamshi ya chuki, udhalilishaji wa thamani na matukufu ya mataifa mengine khususan mataifa ya Kiislamu na pia ni hatua ya kupenda mabavu na kuchochea machafuko.  

Akibainisha kushangazwa na nchi ambayo imekuwa ikidai kutetea haki za wanawake huku ikidai kuwa itaunga mkono haki za wanawake nchini Iran, Kan'ani Chafi ameeleza kuwa hadhi ya mwanake pia imevunjiwa heshima kufuatia kitendo hicho cha utovu wa nidhamu na cha matusi mbali na kudhalilisha thamani na matukufu ya Kiislamu na ya taifa la Iran. 

Katika toleo lake maalumu la Jumatano iliyopita ya Januari 4, jarida hilo la Ufaransa lilifanya kitendo cha kipuuzi cha kuanzisha shindano la kimataifa la michoro na vibonzo, ambapo lilichapisha picha za kuudhi zilizoandamana na maneno, misemo michafu na ya matusi dhidi ya viongozi wa dini. 

Katika mkutano huo wa kila wiki na waandishi wa habari, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amegusia hatua ya serikali ya Iraq ya kutumia neno bandia badala ya neno Ghuba ya Uajemi sambamba na kufanyika mashindano ya nchi za Kiarabu yanayoendelea hivi sasa katika mji wa Basra nchini humo na kueleza kuwa, Iran imewasilisha rasmi malalamiko yake kwa Iraq hasa ikizingatiwa kuwa Ghuba ya Uajemi siku zote itasalia kuwa Ghuba ya Uajemi; na matamshi yanayotolewa na maafisa wa serikali za nchi ajinabi au kuendesha mashindano ya michezo kivyovyote vile haviwezi kubadili uhakika huu wa kihistoria.   

342/