13 Februari 2023 - 16:45
Tathmini ya maandamano ya ‘watu mamilioni moja’ Ufaransa ya kupinga sera za serikali ya Macron

Takribani watu milioni moja waliandamana siku ya Jumamosi nchini Ufaransa ikiwa ni mara ya nne wakipinga sera za serikali ya Rais Emmanuel Macron.

Katika hali ambayo duru ya nne ya maandamano ya nchi nzima ya kuishinikiza serikali ya Macron kuachilia mbali mpango tata wa pensheni ilifanyika juzi Jumamosi, kujitokeza kwa wiki polisi na vikosi vya usalama kwa ajili ya kukandamiza maandamano hayo ya wananchi lilikuwa tukio la aina yake na lililovuta hisia, macho na masikio ya watu. Sambamba na maandamano hayo, polisi na vikosi vya usalama vilimiminika katika miji mbalimbali ya Ufaransa na kutumia mkono wa chuma kukandamiza maandamano hayo ya amani.Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa imetangaza kuwa, zaidi ya watu 960,000 waliandamana siku ya Jumamosi katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. Waandamanaji hao wanataraji kuwa, mashinikizo yao yatazaa matunda na hivyo kumfanya Rais Emmanuel Macron aachane na mpango wake wenye utata wa kuongeza umri wa chini wa kustaafu kutoka miaka 62 hadi 64 kama sehemu ya mpango wa mageuzi.

Umri wa kisheria wa kustaafu nchini Ufaransa kwa sasa ni 62 ambao ni chini kuliko ilivyo katika nchi nyingi zilizoendelea, ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa ya Ulaya na Marekani. Ongezeko la umri wa chini wa kustaafu hadi 64 kutoka miaka 62 ya sasa ni sehemu kuu ya mpango wa mageuzi uliosukumwa na Macron ili kuhakikisha ufadhili wa siku zijazo wa mfumo wa pensheni wa nchi.

Wakati vyama vya wafanyakazi vimekaribisha utayarifu wa serikali kwa mazungumzo kuhusu sehemu za mpango huo, vinasema sheria iliyopendekezwa ya miaka 64 lazima ifutwe. 

Mlolongo wa maandamano hayo umeiweka serikali ya Macron katika mashinikizo makubwa sambamba na migomo katika baadhi ya sekta ambazo zimekuwa zikiungana na waandamanaji. Maandamano yajayo yamepangwa kufanyika tarehe 16 ya mwezi huu. Maandamano ya siku ya Jumamosi katika mji mkuu Paris yanatajwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu yalipoanza maandamnoa ya kupinga mpango wa pensheni wa Rais Macron. Katika baadhi ya maeneo kulishuhudiwa ukandamizaji mkubwa wa polisi dhidi ya waandamanaji. Maandamano hayo yamefanyika siku chache tu baada ya yale ya tarehe 7 mwezi huu.

Yannick Jadot, mmoja wa wanasiasa wa Ufaransa ambaye aligombea pia kiti cha urais katika duru ya kwanza ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter: “Mafanikio ya uhamasishaji dhidi ya mageuzi ya sheria ya kustaafu” na kueleza kuwa, Rais Emmanuel Macron anapaswa kusikia sauti kubwa ya Wafaransa inayopinga mpango wake usio wa kiadilifu na hivyo kuachana nao.”

Elisabeth Borne, Waziri Mkuu wa Ufaransa hivi karibuni alizindua muswada wa mpango wenye utata wa mabadiliko ya sheria ya kustaafu ambao serikali ya Macron imekusudia kuupasisha mwaka huu. Kwa mujibu wa mpango huo, kuanzia mwezi Septemba mwaka huu, serikali ya Paris hatua kwa hatua umri wa kustaafu nchini humo utaongezwa kwa miezi mitatu kila mwaka. Kwa muktadha huo hadi kufikia mwaka 2030 umri wa kustaafu utakuwa miaka 64. Tangu kutangazwa mpango huo wa serikali, kumefanyika maandamano makubwa mawili ya nchi nzima kulalamikia uamuzi huo. Si hayo tu kumekuwa kukifanyika maandamano mengine ingawa sio makubwa kama hayo katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo kupinga sera na uamuzi huu wa serikali ya Macron.

 

Mpango wa kuongeza umri wa kustaafu ulikuwa gumzo na mjadala pia mwaka 2019 na katika mwaka huo ulikabiliwa na upinzani mkali pia. Mpango huo upo katika mkondo na hatua ya kutaka kutekelezwa katika hali ambayo, Ufaransa kama yalivyo akthari ya mataifa ya Ulaya inakabiliwa na matatizo lukuki yanayotokana na vita vya Ukraine kama mfumuko wa bei na kupanda gharama za maisha bila kusahau kupanda pakubwa bei ya chakula na nishati. Licha ya kuwa, Macron anaona kuwa, kufanyika magezui haya ni jambo la dharura na la kiadilifuu, lakini wapinzani wa mpango huo wanasema, kutekelezwa mageuzi haya tena katika kipindi hiki kigumu ni kupuuza majukumu.

Jumuiya za Wafanyakazi nchini Ufaransa zimetangaza mara chungu nzima upinzani wake dhidi ya mpango huo. Wakati sauti za upinzani zikizidi kupazwa, Wizara ya Kazi ya Ufaransa imetangaza kuwa kuongezwa miaka miwili ya umri wa kustaafu na kuwa miaka 64 kutauongezea mfumo wa kustaafu kipato cha Euro bilioni 17 na milioni 700. Hata hivyo, Jumuiya za Wafanayakazi nchini Ufaransa zinasisitiza kuwa, kuna njia nyingine za kudhamini kubakia mfumo wa kustaafu na kuufanya usiyumbe kama kuchukuliwa kodi kutoka kwa matajiri na kuongezwa hisa na kiwango kinachotolewa na waajiri kwa ajili ya pensheni.

Francois Ruffin, mwakilishi wa Bunge la Ufaransa kutoka katika chama cha La France Insoumise anasema: Baada ya miaka mitatu ya janga la corona ambalo limetuchosa wananchi wa Ufaransa, baada ya vita vya Ukraine ambavyo vimewafanya wananchi kushindwa kulipia gharama nyingine kama za nishati huku mishahara ikiwa haitolewi kwa wakati, Rais wa nchi ambaye hakuchaguliiwa kwa hamasa na hakuweza hata kupata wingi mutlaki wa Bunge, baada ya yote haya serikali yake inakuja na mpango mwingine ambao umeiudhi jamii ya Ufaransa.

Kwa msingi huo inawezekana kutabiri kwamba, hali ya mambo hapo baadaye nchini Ufaransa itazidi kuwa mbaya hasa kama mpango wa kuongeza umri wa kustaafu utapasishwa na kutekelezwa. Hii ni kwa sababu tayari wananchi wa nchi hiyo wanataabika kutokana na mlolongo wa mambo ambayo umeyafanya maisha katika nchi hiyo ya bara Ulaya kuwa magumu. Hivyo tutaraji kushuhudia upinzani na malalamiko zaidi ya wananchi katika siku za usoni dhidi ya serikali ya Rais Emmanuel Macron.

342/