15 Februari 2023 - 19:10
Makala ya Raisi katika gazeti la "Wananchi" la China: Marafiki wa zamani ni washirika bora kwa ajili ya mustakbali angavu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha katika makala iliyoandikwa katika gazeti la China la People's Daily ambalo ni gazeti rasmi la Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) kwamba: Tehran na Beijing ni marafiki wa vipindi vigumu na kuandika kuwa: Sera za Iran za kukuza uhusiano wa pande mbili na China zitaendelea bila ya kuathiriwa na matukio ya kikanda na kimataifa.

Makala hiyo ya Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Iran chini ya anwani "Marafiki wa zamani ni washirika bora kwa ajili ya mustakbali mwema" ilichapishwa katika toleo la jana Jumatatu la gazeti la People's Daily la China kabla ya kuanza ziara rasmi ya Rais wa Iran huko Beijing leo Jumanne. 

Rais Raisi ameandika katika makala yake hiyo kwamba: Serikali za Iran na China ambazo zimechagua Mpango wa Ushirikiano wa Pamoja wa Kimkakati kama kigezo cha mahusiano endelevu kati ya pande mbili, zina masuala mbalimbali ya pamoja na yale yenye kushabihiana kuhhusu matukio ya kimataifa. 

Rais Ebrahim Raisi ameandika kuwa, nchi mbili za Iran na China zinapinga hatua za kujitanua na za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kusisitiza  ulazima wa kuheshimiwa haki na maslahi ya nchi zote. 

Makala ya Rais wa Iran katika gazeti la People's Daily la China imeendelea kueleza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga misimamo ya kuchupa mipaka na ugaidi kwa mujibu wa misingi ya Uislamu na kuheshimu dini na tamaduni zote; na inatambua hayo kuwa ni kinyume na Uislamu sahihi na saada ya mwanadamu. Rais Raisi amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuwa na uhusiano mzuri na nchi zote duniani hususan mataifa rafiki kama China. 

342/