5 Machi 2023 - 15:53
Safari ya Grossi mjini Tehran katika kukaribia kikao cha Bodi ya Magavana ya IAEA

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) Ijumaa aliwasili hapa Tehran kwa minajili ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Rafael Grossi amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi kadhaa wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ziara yake ya siku mbili hapa nchini. Behrouz Kamalvandi msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran alisema kabla ya kuanza safari ya Grossi nchini Iran kwamba, "ziara hii inapasa kuwa na manufaa kwa pande zote."    

Grossi pia alisema kabla ya kuanza safari yake mjini Tehran kuwa: "Katika marhala ya sasa; njia ya JCPOA na njia ya pande mbili na Iran haziko katika hali nzuri. Ninataraji kuwa nitaweza kuhuisha, kuratibu tena na kuimarisha mazungumzo haya yasiyoepukika." Bila kazi hii hali itakuwa mbaya zaidi."  

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) katika miaka kadhaa iliyopita umekuwa ukikariri madai yanayotolewa na nchi za Magharibi kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani.  

Kikao cha kwanza cha Bodi ya Magavana ya wakala wa IAEA katika mwaka huu wa 2023 kimepangwa kufanyika Jumatatu Machi 6; ambapo miezi minne iliyopita, bodi hiyo ilipitisha azimio la kuikosoa Iran. Azimio hilo liliitaka Iran kutoa maelezo ya kiufundi kuhusu madai yaliyowasilishwa dhidi yake na pia iandae mazingira na uwezekano wa kufikiwa maeneo na zana ili kukusanya sampuli katika uwanja huo.

Hii ni katika hali ambayo wiki kadhaa zilizopita pia madai mbalimbali kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yamesikika katika vyombo vya habari za Wamagharibi; kitendo kinachoweza kutajwa kuwa ni katika juhudi za nchi za Magharibi za kuandaa mazingira ya kutolewa azimio jingine jipya katika Bodi ya Magavana dhidi ya Iran. Hivi karibuni shirika la habari la Marekani la Blomberg lilitoa ripoti kwa kuwanukuu wanadiplomasia wawili wa ngazi ya juu na kudai kuwa wakaguzi wa IAEA wamegundua chembechembe za urani iliyorutubishwa kwa asilimia 84 wakati walipokagua maeneo ya shughuli za nyuklia ya Iran. Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran aidha amejibu ripoti hiyo ya Blomberg na kusisitiza kuwa Iran haina mradi wa kurutubisha urani kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 60 na kwamba ni jambo la kawaida kupatikana chembechembe hizo ndogo zilizorutubishwa kwa kiwango cha juu katika maeneo kama hayo. 

Wakati huo huo, gazeti la The Wall Street Journal limevinukuu vyombo viwili vya kuaminika na kuripoti kuwa, wakala wa IAEA hauna lengo la kuwasilisha kwa Bodi ya Magavana ripoti huru kuhusu kupatikana katika taasisi za nyuklia za Iran chembechembe hizo tajwa za urani zilizorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 84.   

Kuhusu mazungumzo ya mwisho kati ya Iran na IAEA; Muhammad Eslami Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran pia Jumatano iliyopita aliashiria kuhusu kupatiwa ufumbuzi kadhia zenye kuibua hitilafu na mivutano katika faili la nyuklia na akasema: Ufumbuzi umeshapatikana katika yale masuala ambayo yalitangazwa kwamba hakunda mlandano wa sentrifuji au juu ya uwepo wa chembechembe za urani na kwamba faili limefungwa baada ya kufanyika ukaguzi na imebainika kuwa hakuna ukengeukaji wowote mahsusi uliofanyika. 

Ni dhahir shahir kuwa wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia hadi sasa wametembelea na kukagua mara kadhaa taasisi za nyuklia za Iran lakini hawajawahi kupata ushahidi wala nyaraka zinazothibitisha kuwa miradi ya nyuklia ya Iran inayofanyika kwa malengo ya kiraia imekengekeuka mkondo wa kawaida na inaelekea kuwa ya kijeshi.  

Pamoja na hayo, IAEA hadi sasa imetoa madai mbalimbali mara kadhaa kuhusu miradi ya nyuklia ya amani ya Iran kutokana na mashinikizo kutoka pande za Magharibi na viongozi wa utawala wa Kizayuni; madai ambayo bila shaka hayawiani na rekodi ya ushirikiano kati ya Iran na IAEA. Hii ni kwa sababu, Iran siku zote imekuwa ikitoa mashirikiano chanya kwa wakala huo. 

Katika fremu ya ushirikiano huo, hivi karibuni pia wajumbe wa jopo la ufundi la wakala wa IAEA walifanya safari mara mbili hapa nchini ili kuyapatia ufumbuzi masuala yaliyopo; na wakati huo huo Iran pia ikamwalika Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwa ajili ya ziara hapa Tehran. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa wakala wa IAEA unapasa kutekeleza majukumu yake kiweledi mkabala wa shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya amani; na uache kutumiwa kisiasa na pande za Magharibi au utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Ndio maana Muhammad Eslami Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran akatilia mkazo safari ya Rafael Grossi hapa Tehran. Safari hii inaweza kufungua njia ya kuanza mazungumzo ya JCPOA hata hivyo amesema Iran haikubaliani na mambo yasiyo ya kawaida kiufundi na ambayo ni ya kisiasa na ya utwishaji mashinikizo.

342/