17 Machi 2023 - 22:02
Assad: Nitakutana na Erdogan pale Uturuki itakapoondoka Syria na kuacha kuunga mkono ugaidi

Rais wa Syria ametoa sharti la kukutana na Rais wa Uturuki akisema kuwa atafanya hivyo iwapo nchi hiyo itaondoa wanajeshi wake katika ardhi ya Syria na kusitisha uungaji mkono wake kwa ugaidi.

Jeshi la Uturuki tokea miaka mitatu iliyopita liliyavamia na kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa Syria. 

Damascus imesema kuwa kitendo cha jeshi la Uturuki cha kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Syria ni uvamizi na ukiukaji wa mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo na imetaka kuondoka haraka jeshi la Uturuki katika maeneo hayo. 

Serikali ya Damascus aidha imeeleza kuwa, Uturuki inayasaidia makundi yanayobeba silaha na ya kigaidi katika maeneo yaliyovamiwa na jeshi la nchi hiyo huko kaskazini mwa Syria. 

Rais Bashar al Assad wa Syria amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Sputnik kuhusu uwezekano wa kuonana na Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki katika siku za usoni kuwa, suala la kukutana na kufanya mazungumzo na Recep Erdogan linategemea iwapo Uturuki itakuwa tayari kuondoka kikamilifu katika ardhi ya Syria na kuacha kuunga mkono ugaidi, na wakati hali ya mambo itaporejea katika kipindi cha kabla ya kuanza vita nchini Syria. 

Rais Assad amesisitiza kuwa, kama masharti haya hayajatimizwa kuna faida gani kukutana na kwa nini hilo lifanyike?  

342/