2 Julai 2023 - 22:01
 Machafuko Ufaransa yamlazimu Macron kufuta safari ya Ujerumani huku kijana aliyeuawa akizikwa

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amelazimika kuahirisha ziara yake ya kiserikali nchini Ujerumani ili kusalia mjini Paris ili kukabiliana na maandamano makubwa nchini humo kufuatia kitendo cha polisi kumuua kijana Mfaransa mwenye asili ya Kiarabu aliyetambuliwa kama Nahel M, huku wanafamilia wakimzika kijana huyo.


Macron aliifahamisha Ujerumani siku ya Jumamosi kuwa anaahirisha ziara ya kiserikali ili kujaribu kuzima ghasia zilizoibuka katika maandamano ya wananchi wenye hasira wanaopinga ukatili wa polisi naubaguzi wa kimfumo katika nchi hiyo ya Ulaya ambayo inadai kuwa na mfumo wa kidemokrasia.

Ghasia hizo ambazo zimetikisa nchi hiyo kwa muda wa usiku nne zilizopita zimesababisha hasara kubwa na kusitisha takribani shughul zote nchini humo.

Macron alizungumza kwa njia ya simu na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier "na kumjulisha hali nchini mwake" na kuomba kutoka upande wa Ujerumani kuahirisha ziara hiyo ambayo ilipangwa kuanza leo Jumapili.

Kufutiliwa mbali kwa safari hiyo kunachukuliwa kuwa ni jambo la aibu kwa mtawala huyo wa Ufaransa ambaye mapema mwaka huu alighairi ziara ya kiserikali ya Mfalme Charles III wa Uingereza nchini Ufaransa kutokana na maandamano ya nchi nzima kuhusu mapendekezo yake ya mageuzi ya pensheni.

Maandamano makubwa ya wiki hii pamoja na ghasia za usiku kote nchini yalianza Jumanne baada ya Nahel M aliyekuwa na umri wa miaka 17 kuuawa Juni 29 na polisi katika kituo cha trafiki huko Nanterre, kitongoji cha Paris alikokuwa akiishi.

Katika usiku uliopita, ghasia zililenga maduka na kumbi za miji katika maeneo mbalimbali nchini kote, licha ya wizara ya mambo ya ndani kutuma askari 45,000 wa polisi na pia magari ya kivita kuzima maandamano hayo.

Wakati huohuo, familia ya Nahel ilifanya msafara wa mazishi na maziko siku ya Jumamosi kwenye makaburi ya mtaa huko Nanterre huku umati mkubwa ukihudhuria. Taarifa kutoka katika hafla hiyo zilisema hali ilikuwa ya wasiwasi wakati wa mazishi hayo.

Hafala ya maombolezo pia ilifanyika katika msikiti wa Nanterre kabla ya maziko katika makaburi ya Mont Valerien katika eneo hilo.

Akitoa salamu za rambirambi na kuonyesha mshikamano na familia ya marehemu, Kylian Mbappe, nahodha wa timu ya taifa ya soka ya Ufaransa, anayetoka katika jamii ya wachache nchini Ufaransa, alisema "ameshtushwa na kifo cha kikatili cha kijana Nahel."

 

342/