20 Julai 2023 - 16:59
Sarafu ya dola ya Marekani yaendelea kuporomoka

Taasisi ya Marekani ya Heritage Foundation imetangaza katika ripoti yake ya hivi karibuni na hitimisho lake kuhusu hadhi ya kimataifa wa dola ya Marekani kwamba, sarafu hiyo iko kwenye mkondo wa kushuka na kuporomoka.

The Heritage Foundation, ambayo ni mojawapo ya taasisi za Marekani zenye ushawishi zaidi katika uwanja wa sera za umma, imetangaza katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu hadhi ya kimataifa wa dola ya Marekani kwamba: Serikali ya Marekani imetumia dola kama silaha, na nchi nyingine duniani zinatazama upya misimamo yao juu ya kuendelea kutumia safaru hiyo kwa sababu ya sera hii ya serikali ya Washington.

Kulingana na "Tom Belew", mwanaharakati na mchambuzi wa masuala ya uchumi, mataifa mbalimbali yanaendelea kuachana na matumizi ya dola ya Marekani, hivyo serikali ya Washington inapaswa kuwa makini katika kuendeleza mienendo yake ambayo imepunguza thamani na uaminifu wa mataifa mengine kwa dola ya Marekani.

Wakati huo huo “Raymond Dalio”, bilionea, mwekezaji na mwanaharakati wa uchumi wa Marekani amesema kuhusu suala hili kwamba: Wakati ambapo silaha kubwa ya Marekani ni vikwazo, na serikali ya Washington ina uwezo wa kuzuia mali za watu na nchi nyingine, hakuna sababu ya nchi yoyote kuwa na imani na sarafu ya dola; hivyo inashuhudiwa kwamba, hatua kwa hatua zaidi, shughuli na miamala mikubwa ya kibiashara na kiuchumi duniani inafanyika kwa sarafu nyingine.

Tahadhari hii inatolewa huku nchi mbalimbali zikiendelea kutupilia mbali matumizi ya dola ya Marekani katika miamala yao ya kibiashara.

342/