7 Oktoba 2023 - 17:26
Rais Ebrahim Raisi: Madola yanayowaunga mkono magaidi yanabeba dhima ya shambulizi la Damascus

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililotokea Syria akisema waungaji mkono wa kigeni wa magaidi, wakiwemo wale wanaokalia kwa mabavu ardhi za nchi hiyo, ndio wanaobeba dhima ya hujuma hiyo.

Alhamisi iliyopita makundi ya kigaidi yalishambulia sherehe za kuhitimu masomo maafisa wa chuo cha vita katika mkoa wa Homs (magharibi mwa Syria) kwa kutumia ndege zisizo na rubani.

Wizara ya Afya ya Syria imetangaza watu 89 wameuawa katika shambulizi hilo la kigaidi na 277 wamejeruhiwa.

Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Ijumaa aliandika katika salamu zake za rambirambi kwa Rais, Serikali, jeshi na wananchi wa Syria kwamba: Kuendelea mashambulizi na vitendo vya kigaidi nchini Syria katika miezi ya hivi karibuni ni matokeo ya mwendelezo wa himaya na misaada ya kijasusi, kiusalama na wa zana za kivita kwa magaidi,  lengo likiwa kuzuia juhudi za kurejesha utulivu na usalama kamili katika nchi hiyo.

Sayyid Ebrahim Raisi ameongeza kuwa: Operesheni za magaidi wa Daesh na kitakfiri nchini Syria ni hatua inayokamilisha uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya mamlaka ya kitaifa ya Syria.Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, waungaji mkono wa kigeni wa makundi ya kigaidi, wakiwemo wale wanaoikalia kwa mabavu ardhi za Syria, ambao wanazuia utekelezwaji wa mamlaka ya kitaifa kwenye ardhi yote ya Syria na na kuzuia mapambano madhubuti dhidi ya ugaidi, ndio wanaobeba dhima ya tukio la kuhuzunisha la Damascus. Raisi amebainisha kuwa, jinai hiyo inaonyesha kuwa wapinzani wa usalama, amani na maendeleo katika eneo la Magharibi mwa Asia wanaendeleza mtazamo wao wa kigaidi na kikatili na kusisitiza kuwa, taasisi za kimataifa zinazowajibika, hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zinapaswa kutekeleze wajibu wao katika suala hilo.

342/