Cindy Mcain Mkurugenzi Mtendaji wa WFP ametahadharisha kuhusu maafa ya binadamu katika Ukanda wa Gaza ikiwa ni matokeo ya mzingizo wa pande zote uliowekwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya eneo hilo na kusema: "Watu watakufa njaa tusipoingia katika eneo hilo." Mcain ametahadharisha kuwa: Mzingiro unaoendelea dhidi ya Gaza umewasukuma katika ukingo wa njaa watu milioni mbili na laki tatu wa eneo hilo. Utawala wa Kizayuni wa Israel unalizingira eneo hilo la pwani lenye idadi kubwa ya watu kwa takriban wiki mbili sasa na unajiandaa kwa mashambulizi ya ardhini dhidi ya Gaza kwa kuzidisha mashambulizi yake ya anga. Akiashiria suala hilo katika jarida la Politico linalochapishwa Marekani, Mcain ameongeza kuwa: "Gaza bado inahitaji misaada zaidi. Hivi sasa tunakabiliwa na maafa katika eneo hilo kwa sababu hatuwezi kuwahudumia wakazi wa Gaza, na raia pia hawawezi kupata chochote cha kula; watu hawa watakufa kwa njaa." Wakati huo huo Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa, karibu wakaazi 5,000 wa eneo hilo wakiwemo watoto 1,500 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya Israel. Mkurugenzi Mtendaji wa WFP amegusia pia kuongezeka hatari ya kuenea magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu ikiwa ni matokeo ya kusambaratika miundomisngi ya maji ya watu wa Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa: Hatuwezi kuruhusu siasa zituamulie namna ya kutuma misaada ya kibinadamu, haya ni maafa ya binadamu.
342/