24 Oktoba 2023 - 17:39
Rais Raisi: Msimamo mmoja wa Ulimwengu wa Kiislamu ungeliweza kuzuia dhulma za utawala wa Kizayuni

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: msimamo mmoja wa Ulimwengu wa Kiislamu ungeliweza kuzuia dhulma za wa utawala wa Kizayuni.

Seyed Ebrahim Raisi ameyasema hayo leo katika hafla ya kupokea hati za utambulisho za Abdullah bin Saud Al-Anzi, balozi mpya wa Saudi Arabia mjini Tehran, na akatilia mkazo pia umuhimu wa vyombo vya kidiplomasia vya nchi mbili kufanya juhudi za kutumia zaidi suhula za Iran na Saudia kadiri inavyowezekana kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wenye faida kwa pande mbili na kulinda maslahi ya mataifa ya eneo na Ulimwengu wa Kiislamu. Katika hafla hiyo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa: wakati utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa Magharibi wanatenda jinai zisizo na mfano huko Gaza, msimamo mmoja na kuwa kitu kimoja Ulimwengu wa Kiislamu kungeweza kuzuia kwa namna athirifu zaidi dhulma na uchokozi wa utawala wa Kizayuni na uchu wa kibeberu wa waungaji mkono wake wa Magharibi. Kwa mujibu wa IRNA, Rais Raisi amesema Iran na Saudi Arabia ni nchi mbili kubwa na muhimu katika eneo na akaongeza kuwa: kufaidika kila moja na fursa na uwezo wa upande wa pili na kupanuliwa uhusiano kati ya nchi mbili kutakuwa na taathira chanya katika kustawisha na kuimarisha ushirikiano wa kieneo na kutatua masuala ya eneo na Ulimwengu wa Kiislamu.