Katika muendelezo wa maandamano hayo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, siku ya Jumamosi tarehe 3 Februari baadhi ya walowezi wa Kizayuni walifanya maandamano katikati mwa Tel Aviv kwa lengo la kushinikiza kuharakishwa makubaliano ya kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni.
Maandamano hayo yamefanyika baada ya kushindwa juhudi za utawala wa Kizayuni za kuwakomboa mateka hao kwa kutumia mabavu na kuyashambulia maeneo tofauti ya Gaza. Wiki iliyopita, sambamba na kikao cha baraza la mawaziri la vita la utawala wa Kizayuni cha kujadili kuhusiana na makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, familia za mateka wa Israel zilifanya maandamano mjini Tel Aviv kwa ajili ya kutaka utekelezwaji wa makubaliano ya kubadilishana mateka na kutoa mwito wa kuvunjwa baraza la mawaziri la Netanyahu na kufanyika kwa uchaguzi wa mapema wa Bunge.
Wawakilishi wa utawala wa Kizayuni, Marekani, Misri na Qatar hapo awali walifikia makubaliano mjini Paris, Ufaransa kuhusu fremu ya kusimamisha vita na kuwaachia huru mateka wengine wa jeshi la utawala huo ghasibu wa Israel na Hamas.Harakati mbili za Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Jihadul Islami zimesema kuwa, mapendekezo yoyote ambayo hayatopelekea kusimamishwa kikamilifu uvamizi wa Israel huko Gaza, hayakubaliki kwa namna yoyote ile.
Hamas na Jihadul Islami zinasisitiza kuwa, mazungumzo yoyote ambayo hayatopelekea kumalizwa vita na kuondoka wanajeshi vamizi wa Israel nje ya Ukanda Gaza pamoja na kuhitimishwa mzingiro na kujengwa upya ukanda huo hayawezi kukubaliwa na harakati hizo, na hakuna mabadilishano yoyote ya mateka maadamu masharti hayo hayajatimia.
Maandamano dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Neytanyahu yamekuwa yakiendelea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na ambazo zimepewa jina bandia la Israel tangu Oktoba 7 mwaka jana (2023) wakati kulipotekelezwa na muqawama operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa.
Waandamanaji hao wanasisitiza kuwa, baraza la mawaziri la Netanyahu limeshindwa kuwarejesha mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa na Hamas. Mamlaka za utawala wa Kizayuni huficha takwimu kamili za wafungwa wao wa kijeshi, lakini idadi yao inakadiriwa kuwa ni mamia.
342/