Wakati huo huo, Russia inakusudia kuimarisha zaidi vikosi vyake vya kimkakati vya nyuklia ili kukabiliana na ongezeka la misimamo ya uhasama ya shirika la NATO linaloongozwa na Marekani.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetangaza kuwa, jeshi la Ukraine linaruhusiwa kutumia makombora ya masafa marefu ya Marekani kushambulia maeneo ya ardhi ya Russia. Msemaji wa Pentagon, Patrick Ryder, alidai kuwa Russia inatumia ardhi yake kama "eneo salama" na kushambulia maeneo ya Ukraine kutoka ndani ya mipaka yake. Aliongeza kuwa: "Kwa kuwa tumeshuhudia operesheni kama hii ya vikosi vya Russia, tumeitangazia Ukraine kwamba inaweza na ina haki ya kujibu mashambulizi haya kwa ajili ya kujilinda." Hata hivyo, Pentagon ilidai kuwa idhini hii haina maana ya kupitishwa sera mpya.
Maafisa wa Ukraine wametangaza kuwa, Marekani imebana matumizi ya silaha hizo kulenga shabaha umbali wa chini ya kilomita 100 kutoka mpakani. Maafisa wa serikali ya Marekani wamekataa kuthibitisha habari hii. Wakati huo huo, Ikulu ya Rais wa Marekani ilitangaza Alhamisi iliyopita kuwa, inapanga kuharakisha mpango wa kupeleka mifumo ya ulinzi wa anga huko Ukraine. Hapo awali Marekani iliipatia Ukraine mifumo ya ulinzi wa anga, ikiwa ni pamoja na Patriot na mfumo wa kujikinga na makombora wa NASAMS.
Vitendo vya uchochezi na vya kichokozi vya Washington dhidi ya Moscow kwa kutoa idhini kwa Kiev kushambulia ardhi ya Russia kwa makombora ya Marekani vinafanyika ili kuidhoofisha nchi hiyo kadiri iwezekanavyo, haswa katika suala la kijeshi, na pia kusababisha uharibifu mkubwa zaidi kwa miundombinu ya kijeshi na viwanda vya Russia katika maeneo ya mbali. Marekani na NATO, ambazo zimetuma zaidi ya dola bilioni mia moja za msaada wa kijeshi na silaha kwa Ukraine, bado zinataka kuendeleza vita vya umwagaji damu nchini Ukraine kwa lengo la kuidhoofisha Russia kadiri inavyowezekana.
Wakati huo huo, NATO pia imezidisha sera zake za kivita dhidi ya Russia. Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, ameeleza kwamba muungano huo wa kijeshi wa Magharibi unapingana na Russia na China, na kutangaza kwamba wanachama wa NATO wameanza harakati za maandalizi ya kukabiliana na silaha za nyuklia. Katika suala hili, NATO inafanya mazungumzo na nchi wanachama ili kuweka tayari vichwa vya silaha za nyuklia kwa ajili ya uwezekano wa kukabiliana na Russia na China. Stoltenberg alidai kuwa vitisho vya China na Russia vimeongezeka.
342/