Anwar ameyasema hayo katika hafla ya ufunguzi wa Msikiti Mkuu wa Malaysia mjini Kuala Lumpur, ambapo mbali na kubainisha kuwa, ulimwengu wa Magharibi unapaswa uache hatua zake za kujaribu kudhibiti na kuviongoza vyombo vya habari vya kimataifa ili vitoe "simulizi zisizo sahihi" kuhusu vita vya Ghaza amesisitiza kwamba hakuna ulazima kwa Magharibi kuufundisha Ulimwengu wa Kiislamu maana ya demokrasia, haki za binadamu na ustawi endelevu.
Waziri Mkuu wa Malaysia amesema: hali ya kukoseakana utulivu Palestina haikutokana na operesheni ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba, bali ilianza mwaka 1948 na imekuwa ikiendelea tangu wakati huo hadi sasa.
Anwar ameongeza kuwa: Malaysia imesha ahidi kuwa haitatoa kibali kwa makampuni yaliyosajiliwa Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu) kuingia nchini humo na kufanya shughuli zozote zile.
Anwar Ibrahim ametangaza msimamo huo wakati nchi yake na Brunei zikitoa kauli ya kulaani mauaji ya kimbari na ukatili unaoendelea kufanywa huko Ghaza na utawala ghasibu wa Kizayuni na kueleza wasiwasi mkubwa walionao kutokana na hali ya eneo hilo.
Katika mkutano wa kila mwaka wa viongozi wa nchi hizo mbili, Sultani Hassanal Bolkiah wa Brunei na Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim wameeleza wasi wasi mkubwa walio nao kuhusu hali mbaya ya Asia Magharibi na kulaani mauaji ya kimbari na uchokozi unaoendelea kufanywa katika Ukanda wa Ghaza na utawala haramu wa Kizayuni, ambao umesababisha maafa ya kibinadamu na kuteketea roho nyingi za watu.
Aidha, viongozi wa nchi hizo mbili wamesisitiza uungaji mkono wao kamili wa kuanzishwa taifa huru la Palestina kwa kuzingatia mipaka ya kabla ya 1967 na mji mkuu wake ukiwa ni Baitul-Muqaddas Mashariki.
Wapalestina wasiopungua 40,405 wameuawa shahidi hadi sasa na wengine wapatao 93,468 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoanzisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza.../
342/