12 Septemba 2024 - 12:48
Zaidi ya watu 150 wapoteza maisha kwa kimbunga kilichosababisha mafuriko Vietnam

Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na kimbunga Yagi imeongezeka hadi 152 nchini Vietnam, kulingana na makadirio ya serikali, huku moja ya mito mikubwa nchini humo ikifikia kiwango chake cha juu zaidi katika miongo miwili.

Kufikia Jumatano, maji ya mafuriko kutoka kwenye Mto Mwekundu yalifikia urefu wa mita katika sehemu za mji mkuu, na kuwalazimu wakazi wengine kuzunguka vitongoji vyao kwa mashua.

Ripoti zinasema kuwa, maelfu ya watu wamehama kutoka maeneo ya tambarare ya jiji na wilaya 10 kati ya 30 za utawala za mji mkuu Hanoi ziko kwenye "tahadhari ya mafuriko".

Duru za serikali zinasema kuwa, mafuriko na maporomoko ya udongo katika maeneo ya kaskazini mwa Vietnam yamekuwa sababu kuu za vifo kutokana na kimbunga hicho."Haya ndiyo mafuriko mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa," mkazi wa Hanoi Tran Le Quyen aliambia shirika la habari la Reuters.

"Nyumba yangu sasa ni sehemu ya mto," Nguyen Van Hung, ambaye anaishi katika kitongoji kwenye kingo za Mto Mwekundu, aliiambia Reuters.

Kijiji kizima katika jimbo la kaskazini la Lao Cai kilisombwa na maji siku ya Jumanne huku kukiwa na mafuriko. Takribani watu 25 wamethibitishwa kufariki, na mamia ya wanajeshi wametumwa katika kijiji hicho kuwatafuta wale ambao bado hawajapatikana.

Mamlaka pia inazingatia kwa uangalifu mtambo wa kufua umeme katika mkoa wa Yen Bai kaskazini-magharibi, kwani uingiaji mkubwa wa maji kwenye bwawa linalozunguka bwawa hilo unazua wasiwasi kwamba huenda likaporomoka. Ikumbukwe kuwa, kabla ya kupiga Vietnam, kimbunga hicho kilisababisha vifo vya watu 24 kusini mwa China na Ufilipino. 


342/