Rais Pezeshkian amepangiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa ya Iran siku ya Jumanne ambapo mbali na hutuba hiyo atashiriki pia katika kikao cha viongozi wa Agano la Baadaye, kukutana na kuzungumza na baadhi ya wakuu wa nchi zinazoshiriki kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, makundi ya kisiasa, kijamii, kidini na vyombo vya habari na watu binafsi nchini Marekani kwa ajili ya kuweka wazi misimamo ya Iran na kujibu maswali mbalimbali yanayohusiana na Iran.
Kabla ya kuelekea New York, Dakta Pezeshkian amewaambia waandishi wa habari kwamba atakutana na Wairani wanaoishi Marekani kwa madhumuni ya kushauriana nao na kukurubisha pamoja mitazamo ya pande mbili. Amesema Umoja wa Mataifa ni moja ya matokeo muhimu ya juhudi za mwanadamu, na kuwa iwapo utatekeleza majukumu yake inavyopaswa, nchi moja haiwezi kuishambulia nchi nyingine kwa mabomu kwa kutegemea nguvu zake za kijeshi bila sababu ya kisheria. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amebainisha kwamba Iran ni salama na huru kuliko vile inavyodhihirishwa na kuchafuliwa jina katika televisheni za kigeni na kwamba Iran ni ya Wairani wote.
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alimtangulia Rais Pezeshkian mjini New York, ambapo amekutana na kuzungumza na baadhi ya maafisa wa Umoja wa Mataifa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mbalimbali. Katika vikao hivyo, Araghchi amefafanua misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na matukio ya kimataifa na kieneo, yakiwemo ya Ukanda wa Gaza.
Katika miaka ya hivi karibuni marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakishiriki katika vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakiandamana na ujumbe wa wanadiplomasia na mawaziri wa mambo ya nje kwa madhumuni ya kubainisha misimamo ya Iran kuhusiana na matukio muhimu ya kieneo na kimataifa. Rais Masoud Pezeshkian pia atafafanua vipaumbele muhimu zaidi vya siasa za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko New York, kwa kuzingatia matukio ya hivi sasa kieneo na kimataifa.
Safari ya Pezeshkian mjini New York na hotuba yake katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa inaweza kuwa moja ya mafanikio muhimu ya serikali ya awamu ya 14 katika siku zake za mwanzo kazini, ambapo mazungumzo na mikutano ya wajumbe alioandamana nao inaweza kuandaa uwanja wa kuondolewa baadhi ya vikwazo vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran.
Safari hii pia inalenga kupanua ushirikiano wa Iran na nchi nyingine katika uga wa teknolojia na uchumi. Kwa kuzingatia mazungumzo yatakayofanyika New York, kuna uwezekano wa kuandaliwa uwanja wa kuletwa nchini teknolojia mpya kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika nyanja mbalimbali za viwanda.
Moja ya maudhui muhimu za safari ya Pezeshkian mjini New York ni kujadili suala la vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na serikali za Magharibi dhidi ya Iran na nchi nyinginezo huru. Kukabiliana na misimamo ya upande mmoja ya Washington na taathira hasi za vikwazo pia ni masuala muhimu na ya msingi ambayo Rais wa Iran atayashughulikia katika safari yake hiyo.
Rais Pezeshkian pia atafichua katika jukwaa la Umoja wa Mataifa uungaji mkono wa wale wanaodai kuteteta haki za binadamu kwa makundi ya kigaidi dhidi ya taifa la Iran, kuweka wazi uzingatiaji wa haki za binadamu nchini Iran na kutetea haki zinazokiukwa za taifa la Iran katika ngazi za kimataifa.
Mada nyingine ya hotuba ya Rais Pezeshkian itahusu matukio ya eneo na hali ya sasa ya Ukanda wa Gaza. Jinai za utawala wa Kizayuni na vitendo vya jinai na kigaidi vya Wazayuni dhidi ya watu wa Palestina na Lebanon ni masuala mengine muhimu ambayo rais huyo atayagusia katika hotuba yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Nukta nyingine muhimu kuhusu safari ya Rais Pezeshkian mjini New York ni kukutana na Wairani wanaoishi Marekani. Kunufaika na uwezo wa Wairani walio nje ya nchi na kuvutia mitaji na uwekezaji wao wa kisayansi na kiuchumi pia imekuwa sehemu muhimu ya siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na sera za marais waliopita katika vipindi tofauti vya uongozi wao na kubainishwa wazi wakati wa kushiriki kwao katika vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
342/