Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Hizbullah ilisema kuwa ilishambulia kwa mabomu majengo ya viwanda vya kijeshi vya kampuni ya Rafael, iliyoko katika eneo la Zevulun kaskazini mwa Haifa.
Harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon imebainisha kuwa operesheni yake ni kielelezo cha uungaji mkono kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na mapambano yao, na vilevile ni "jibu la awali kwa mauaji ya kikatili yaliyofanywa na adui Muisraeli katika maeneo mbalimbali ya Lebanon" kwa kulipua vifaa vya mawasiliano.
Maelfu ya vifaa vya kielektronikki vya mawasiliano hasa 'pager' na redio za mawasiliano-walkie-talkie za wanachama wa Hizbullah zililipukaa nchini Lebanon katika milipuko ya wakati mmoja Jumanne na Jumatano, na kuua watu 42 na kujeruhi karibu wengine 3,500.
Uchunguzi wa awali wa mamlaka ya Lebanon umegundua kuwa vifaa hivyo viliwekwa vilipuzi kabla ya kuwasili katika nchi hiyo ya Kiarabu na kwamba vililipuliwa kupitia jumbe za kielektroniki.
Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zimesema shambulio hilo kubwa la kigaidi lilitokana na ushirikiano wa pamoja wa jeshi la Israel na shirika la kijasusi la utawala huo, Mossad.
Hizbullah imeapa kulipiza kisasi dhidi ya utawala ughasibu wa Kizayuni, ambao pia unaendesha vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.
Kampuni ya Rafael iliyolengwa katika operesheni ya Jumapili ya Hizbullah ni mojawapo ya wazalishaji watatu wakubwa wa silaha wa Israel na inamilikiwa na utawala huo haramu.
Rafael huzalisha mifumo ya magari ya kivita, mifumo ya Kuba la Chuma la David (Iron Dome David), na aina mbalimbali za makombora.
342/