2 Oktoba 2024 - 20:06
Utendaji mpya wa Ansarullah ya Yemen dhidi ya Israeli; sasa ni jicho kwa jicho

Katika kukabiliana na mashambulio mapya ya utawala wa Kizayuni dhidi ya taasisi mafuta na bandari za Yemen, Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetishia kushambulia maeneo ya raia huko Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu).

Duru za habari zimetangaza kuwa, Jumapili jioni ndege za kivita za Israel zililenga matangi ya mafuta katika bandari ya Ras Issa na bandari ya Al-Jadidah katika Bahari Nyekundu magharibi mwa Yemen.

Bandari ya Ras Isa, ambayo iko katika ufuo wa Bahari Nyekundu na mkoa wa Hudaidah, ni moja ya vituo vikuu vya kuhamisha mafuta ghafi ya Yemen hadi katika masoko ya kimataifa. Hapo awali, bandari hii ilikuwa ikitumika zaidi kusafirisha mafuta, lakini sasa Wayemeni wanaitumia kupakua na kuhifadhi mafuta.

Hili ni shambulio la pili la utawala wa Kizayuni dhidi ya Yemen katika kipindi kisichozidi miezi miwili. Mwezi Julai, ndege za kivita za Israel zililenga maeneo ya karibu na Hudaidah baada ya ndege isiyo na rubani ya Yemen kulenga Tel Aviv.

Jumapili usiku, duru za kitiba za Yemen zilichapisha takwimu za hivi karibuni kabisa za majeruhi wa mashambulizi ya siku ya Jumamosi ya utawala wa Kizayuni huko Hudaidah, ambapo watu watano waliuawa shahidi na wengine 45 kujeruhiwa.

Katika kujibu mashambulizi hayo, afisa mmoja mwenye mfungamano na Ansarullah amesisitiza kuwa, hatua ya adui ya kushambulia raia nchini Yemen haitaachwa bila majibu na kwamba, Wazayuni wanapaswa kulijua hilo.

Kabla ya hapo Ansarullah ya Yemen imekuwa ikilenga shabaha mara kwa mara maeneo ya kijeshi ya utawala huo ghasibu katika kukabiliana na mashambulizi na jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon, licha ya utayari wa mifumo ya ulinzi ya utawala huo na hivyo kudhihirisha wazi udhaifu wa mifuumo ya kiulinzi ya utawala huo ghasibu.

Huko nyuma, makundi ya muqawama yakiwa na lengo la kushikamana na misingi ya kimaadili na kanuni za vita, yamekuwa yakishambulia zaidi maeneo ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni katika mashambulizi ya kulipiza kisasi na kuepuka kuwalenga raia.

Lakini kuendelea kwa mashambulizi ya utawala huo katili dhidi ya raia na kukanyaga misingi na sheria za vita kumeyaweka makundi ya upinzani katika hali ambayo yumkini yakabadilisha mtazamo wao ili kuweka uwiano mpya, na inaonekana kuwa, makundi mengine ya muqawama pia yatakuwa hayana budi isipokuwa kuangalia upya utendaji wao wa hapo kabla kama ilivyofanya Ansarullah ya Yemen.

Kinachoonyesha kubadilika kwa mtazamo wa Ansarullah ni ukweli kwamba Wayemen wana uwezo mkubwa sana wa makombora na ndege zisizo na rubani, ambapo wameonyesha tangu mwanzo wa vita vya Gaza, na wakati huo huo, kwa kuitungua ndege nyingine isiyo na rubani ya MQ-9 ya Marekani katika mkoa wa Saada, pia wamedhihirisha uwezo wao wa ulinzi wa anga.

Ansarullah imelenga zaidi ya meli 80 kwa makombora na ndege zisizo na rubani tangu kuanza kwa vita vya Gaza.

Yemen imejulikana kwa muda mrefu kwa uwezo wake wa makombora, katika uwanja wa makombora ya kujihami na katika uga wa makombora ya kushambulia na kwa kweli, jeshi la nchi hiyo linaweza kuwekwa katika fremu nguvu ya makombora.

Ni uwezo huo na woga wa uwezo wa makombora wa Yemen ulioilazimisha Marekani kufanya mazungumzo ya siri kati ya mwaka 2004 na 2007 na Rais wa wakati huo wa Yemen Ali Abdullah Saleh ili kupunguza uwezo wa makombora wa nchi hiyo hususan katika uga wa makombora ya ulinzi mkabala wa kupatiwa fedha  ili kwa njia hiyo idhoofishe uwezo wa makombora wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Uwezo huu mkubwa wa makombora wa jeshi la Yemen, ambao ulifikiwa kwa miongo kadhaa, baada ya serikali mpya ya Yemen kuchukua madaraka, sekta ya makombora ya nchi hiyo ilichukua mkondo mpana zaidi na kivitendo kukawa kumetokea mapinduzi ya makombora katika muundo wa kijeshi wa nchi hiyo.

Ukweli wa mambo ni kuwa, jeshi lililoundwa upya la Yemen, lilifanikiwa kupata mafanikio makubwa kwa mhimili wa vikosi vya Ansarullah baada ya kutengeneza  makombora mbalimbali ya masafa marefu, masafa ya kati na masafa mafupi pamoja na mfumo wa ulinzi wa ardhini hadi angani na wa ardhini hadi baharini. Makombora hayo yalitumiwa kulenga ngome za nchi wanachama wa muungano wa Saudia hususan ndani ya Saudi Arabia na Imarati ambapo hatimaye hilo lilizilamisha nchi hizo kubadilisha utendaji wao wa kijeshi nchini Yemen na kwa uwezo huu huu wanamuqawama wa Yemen wanaweza kuupigisha magoti utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hivi sasa jeshi la Yemen lina wigo mpana wa makombora ya balistiki na ya cruise jambo ambalo linahesabiwa kuwa tishio kubwa ndani ya ardhi ya maadui zake ukiwemo utawala wa Kizayuni na kwa kuzingatia eneo maalumu la kijiografia la Yemen na udhibiti wake, baadhi ya mishipa mikuu ya uchumi wa dunia kama Ghuba ya Aden, Lango Bahari la Bab al-Mandab na sehemu kubwa ya Bahari Nyekundu, Yemen inaweza kwa urahisi kwa kutumia makombora hayo na kivitendo kuwapa changamoto maadui zake, kama ambavyo katika miezi ya hivi karibuni ikituumia uwezo huu huu wa kijioarafia na kijeshi imetoa pigo kubwa kwa uchumi wa utawala haramu wa Israel na kuuweka katika hali ambayo ambayo haijawahi kushuhudiwa katika sekta ya nishati na vilevile katika uga wa kudhamini mahitaji ya chakula.

342/