21 Januari 2025 - 19:44
Nyaraka zavuja kuhusu msaada wa mafuta wa Erdogan kwa utawala wa Israel

Mbunge wa Uturuki amewasilisha picha za satalaiti na nyaraka za data za baharini katika bunge la nchi hiyo zinazothibitisha kwamba Ankara imekuwa ikitoa msaada wa mafuta kwa utawala wa Israel.

Kwa mujibu wa video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya taarifa iliyotolewa na mbunge wa Uturuki, Ömer Faruk Gergerlioğlu, nchi hiyo ni miongoni mwa wasambazaji wakuu wa mafuta kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katikati ya mwezi Disemba mwaka jana, Ömer Faruk Gergerlioğlu alisema katika Bunge la Uturuki kwamba: "Meli zetu zilizima alama za ishara za eneo zilipokuwa na kuonyesha kuwa zinaelekea Italia, lakini tulichunguza picha za satalaiti ambazo zilionyesha kuwa meli za mafuta za Nissos Delos na Seavigor zilikwenda kwenye bandari za Haifa na Ashdod katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina."

Hapo awali, ripoti ya Taasisi ya Takwimu ya Uturuki ilionyesha kuwa, serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan ilikuwa imeuuzia silaha utawala wa Israel katika kilele cha mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Uturuki ilikuwa nchi ya kwanza ya Kiislamu kuutambua utawala wa ghasibu wa Israel na kuanzisha uhusiano wa pande mbili na utawala huo.

Rais Erdogan wa Uturuki pia alikuwa kiongozi wa kwanza Muislamu kuzuru kaburi la Theodor Herzl, mwasisi wa Uzayuni, katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

342/