9 Machi 2025 - 22:18
Source: Parstoday
UN: Utawala wa Trump uache kuingilia uhuru wa mahakama

Ripoti Maalumu wa Umoja wa Mataifa amekosoa vikali hatua za hivi majuzi za serikali ya Donald Trump ya kuwatimua na kuwateua maafisa wapya wa mahakama, akielezea wasiwasi wake kwamba hatua hizi ni sehemu ya vitisho kwa uhuru wa mfumo wa mahakama wa Marekani.

"Tangu utawala mpya wa Marekani ulipoingia madarakani Januari 20, 2025, idadi kubwa ya mawakili, waendesha mashtaka na majaji wanaoshughulikia kesi za uhamiaji wamepewa kazi nyingine, kuhamishwa au kufutwa kazi bila taratibu za kawaida," amesema  Margaret Satterthwaite, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhuru wa Majaji na Mawakili.

Ameongeza kuwa mawakili walioathiriwa na hatua hizo ni pamoja na waendesha mashtaka wengi katika Idara ya Sheria ya Marekani ambao walifutwa kazi baada ya kushiriki katika uchunguzi wa jinai dhidi ya Trump au uvamizi wa wafuasi wake wa Januari 6, 2021 kwenye Bunge la Marekani.

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa pia ameongeza kuwa: "Tangu baada ya kufutwa kazi wanasheria na mawakili hao, waendesha mashtaka kadhaa wa Wizara ya Sheria wamejiuzulu. Hatua hizi zimetumika kama silaha dhidi ya maafisa wa serikali iliyopita."

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa ameendelea kusema: “Nina wasiwasi sana kwamba hatua hizi ni sehemu ya vitisho vinavyoendelea kutolewa kwa wataalamu na uhuru wa mahakama.”

 Margaret Satterthwaite ameendelea kusema: "Serikali ya Marekani lazima ikomeshe uingiliaji wake katika masuala ya mahakama na kuhakikisha kwamba siasa hazina nafasi katika mfumo wa mahakama."

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha