Taarifa ya Hamas imebainisha kuwa: Kuuawa shahidi Esmail Barhoum ni jinai nyingine katika rekodi nyeusi ya utawala wa Kizayuni inayoonyesha kuendeleza kutekelezwa sera za mauaji ya kigaidi dhidi ya raia na viongozi wa Palestina.
Taarifa ya Hamas imesisitiza kuwa shambulio hilo limekiuka wazi sheria na kanuni za kimataifa; na harakati hiyo inaihesabu hatua hiyo kuwa ya hatari sambamba na jinai za kivita za utawala wa Kizayuni.
Hamas imeashiria nafasi kuu ya shahidi Barhoum katika harakati za Kiislamu na za muqawama na kumtaja kuwa miongoni mwa shakhsia mashuhuri wa harakati ya Hamas huko Gaza na kusisitiza kuwa alitumia maisha yake yote kuhami Palestina, matukufu yake na taifa lake.
Esmail Barhoum mwakilishi wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas aliuawa shahidi jana Jumapili katika shambulio la utawala wa Kizayuni katika hospitali ya al Nasser huko Gaza.
Kufuatia mauaji hayo, Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina pia imeeleza kuwa: Wanamapambano katika Ukanda wa Gaza wanajivunia viongozi wao wanaouliwa shahidi kwa kuendesha mapambano na kusimama kidete kuitetea Palestina.
Usiku wa kuamkia jana pia Jeshi la Israel lilifanya mashambulizi mapya ya kutisha ya anga katika Ukanda wa Gaza na kuua shahidi watu wasiopungua 40, akiwemo Salah al-Bardawil, Mbunge wa Palestina na Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas.
342/
Your Comment