26 Machi 2025 - 15:20
Source: Parstoday
Kashfa ya usalama wa Marekani; taarifa nyeti za kijeshi kuhusu Yemen zavuja

Kosa kubwa la utawala wa Trump katika kutumia mtandao usio na usalama kabla ya kuishambulia Yemen limezusha wimbi la wasiwasi katika duru za kisiasa na kijasusi za nchi hiyo.

Jeffrey Goldberg, mhariri mkuu wa The Atlantic, alitangaza Jumatatu kwamba alijumuishwa kwa sadfa kwenye kundi moja la mtandao wa Signal ambako baadhi ya maafisa wakuu wa serikali ya Marekani walikuwa wakipeana habari kuhusu operesheni za kijeshi za nchi hiyo dhidi ya Yemen.

Goldberg amesema kuwa, alikuwa na habari kamili kuhusu majadiliano yaliyojiri kati ya maafisa wakuu wa serikali ya Marekani juu ya mashambulizi dhidi ya Yemen masaa mawili kabla ya kuanza mashambulizi hayo.

Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Ikulu ya Rais wa Marekkani, White House, Michael Waltz alianzisha mazungumzo kupitia mawimbi ya programu ya ujumbe uliosimbwa katika mtandao wa Signal. Kundi lililoshiriki mazungumzo hayo lilijumuisha Waziri wa Ulinzi, Mshauri wa Usalama wa Taifa, Waziri wa Mambo ya Nje, Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa, na maafisa wengine wakuu wa serikali ya Marekani.

Washiriki katika mazungumzo hayo walijadili ulazima wa kufanya mashambulizi dhidi ya Yemen na sababu za utawala wa Trump za kufanya hivyo.

Kuvuja kwa taarifa hizi kumeibua wasiwasi kuhusu kiwango cha usalama wa mawasiliano ya maafisa wa serikali ya Marekani na utumiaji wao wa mitandao isiyo na usalama kwa ajili ya kupanga mipango ya kijeshi.

Ripoti zinasema, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Peter Brian Hegseth  amefichua maelezo ya operesheni za kijeshi ambayo yanaweza kuweka maisha ya Wamarekani hatarini. Sasa waziri huyo yuko chini ya uchunguzi mkali na ufuatiliaji wa kosa hili kubwa.

Kashfa ya usalama wa Marekani; taarifa nyeti za kijeshi kuhusu Yemen zavuja

Ripoti nyingine zinasema huenda Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Ikulu ya Rais wa Marekani, Michael Waltz, akalazimika kujiuzulu kutokana na mashinikizo makubwa ya kisiasa yaliyosababishwa na kashfa hiyo.

Tangu tarehe 15 mwezi huu wa Machi, Marekani ilianzisha mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen katika mikoa mbalimbali ya nchi hiyo. Mashambulizi haya yanafanyika ili kuizuia Yemen kuwatetea watu wa Palestina hususan huko Gaza wanaoendelea kuuawa kinyama na utawala ghasibu wa Israel.  

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha