Lebanon ina mpaka wa kijiografia na utawala huo ghasibu unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu. Utawala huo ghasibu daima umekuwa na tamaa ya kutaka kukalia kwa mabavu ardhi ya Lebanon. Katika miaka ya 1980, utawala wa Kizayuni uliteka maeneo ya kusini mwa Lebanon, ambapo hatimaye ulilazimika kuondoka kwenye eneo hilo kwa madhila mwaka 2000 kutokana na muqawama wa vikosi vya Hizbullah. Uwepo wa Hizbullah katika uga wa kisiasa na kijeshi wa Lebanon daima umekuwa kikwazo kikubwa katika kufikiwa malengo ya utawala huo wa kibaguzi.
Nafasi ya Hizbullah katika medani ya kisiasa ya Lebanon bila shaka ni kikwazo kikubwa mkabala wa tamaa na siasa zozote za utawala wa Kizayuni za kutaka kuwa na uhusiano wa kawaida na Lebanon. Kufuatia kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, hayati Katibu Mkuu wa Hizbullah nchini Lebanon na utawala huo mnamo Septemba 2024, na pia kuingia madarakani huko Marekani Raid Donald Trump, dalili zimeanza kuibuka za juhudi zinazofanywa na Tel Aviv na Washington kwa ajili ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kati ya utawala wa Kizayuni na Lebanon.
Dhana ya utawala wa Kizayuni na Marekani ni kwamba kukiwa na rais na waziri mkuu mpya nchini Lebanon, kuna uwezekano wa kuanzishwa uhusiano wa aina hiyo kati ya pande mbili. Kuhusiana na hilo, katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita kumechapishwa ripoti kadhaa kuhusu mienendo ya kutiliwa shaka ya Marekani na utawala wa Kizayuni ya kujipenyeza katika medani ya kisiasa ya Lebanon kwa kutumia vibaya udhaifu wa serikali na rais wa nchi hiyo. Gazeti la Al-Akhbar limeoonya katika moja ya ripoti zake kwamba Marekani inataka kuwahimiza wanadiplomasia na wanasiasa wa Lebanon washiriki katika mikutano ya moja kwa moja na maafisa wa Israel mbele ya wawakilishi wa Marekani na Ufaransa.
Mjumbe wa Rais Donald Trump wa Marekani katika eneo hilo, Steven Witkoff hivi karibuni alielezea matumaini yake kuhusu uwezekano wa Saudi Arabia kujiunga na mapatano ya maridhiano na Israel, akisema kwamba matukio ya kisiasa katika eneo hilo yanaweza pia kuijumuisha Lebanon na Syria, na kwamba Lebanon hivi karibuni itaingia kwenye mkondo wa makubaliano ya maridhiano na Israel, kama ambavyo Syria pia inasemekana kuwa kwenye mkondo huo huo. Hata hivyo, juhudi hizi zinaonekana kutokana na Washington na Tel Aviv kutoelewa vizuri hali ya kisiasa ndani ya Lebanon. Hizbullah inafadhilisha kuwa na subira wakati huu ili kuzuia vita vingine, lakini subira na kimya hiki kamwe hakimaanishi kwamba itaendelea kukaa kimya mbele ya masuala ya kufedhehesha na kutovumilika kama juhudi za kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.
Mbali na Hizbullah, kuna makundi mengine ya kisiasa huko Lebanon ambayo hayakubali kabisa kuanzishwa uhusiano na utawala wa Kizayuni. Mbali na makundi ya kisiasa, sehemu kubwa ya wananchi wa Lebanon pia inapinga vikali kuanzishwa uhusiano na utawala wa Kizayuni. Kwa hakika kuchukizwa Walebanon na utawala wa Kizayuni na kuuona kuwa utawala wa kivamizi unaotenda jinai za kutisha dhidi ya watu wasio na hatia, ni sehemu ya utambulisho wa watu waliowengi wa Lebanon.
Ni kwa kuzingatia hali hiyo, ndipo Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon akafichua kwamba adui Mzayuni anakusudia kuiburuza Lebanon katika mazungumzo ya kisiasa ambayo yatapelekea kuanzishwa uhusiano kati ya pande mbili hizo, suala ambalo amesisitiza kuwa Walebanon hawako tayari kulikubali.
342/
Your Comment