5 Aprili 2025 - 23:36
Source: Parstoday
Wanazuoni wa Kiislamu watoa fatwa; Mataifa ya Kiislamu yaunge mkono Muqawama wa Palestina

Umoja wa Kimataifa wa Wanazuoni wa Kiislamu (IUMS) umetoa fatwa (agizo la kidini) ukizitaka nchi za Kiislamu kutoa msaada wa haraka wa kijeshi, kifedha na silaha kwa mrengo wa Muqawama wa Palestina, ili kukabiliana na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala katili wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Fatwa hiyo ambayo imeidhinishwa na zaidi ya wanazuoni 10 mashuhuri duniani, inataka uingiliaji wa moja kwa moja wa kijeshi, vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Israel, na kuungwa mkono zaidi kwa makundi ya Muqawama ya Wapalestina.

Aidha inataka kubuniwa muungano wa kijeshi wa Kiislamu kwa shabaha ya kuyalinda mataifa ya Kiislamu na kukabiliana na uvamizi wa kigeni.

"Kushindwa kwa serikali za (nchi za) Kiarabu na Kiislamu kuunga mkono Gaza wakati inasambaratishwa kunachukuliwa na sheria za Kiislamu kuwa jinai kubwa dhidi ya ndugu zetu wanaokandamizwa huko Gaza," amesema Ali al-Qaradaghi, Katibu Mkuu wa muungano huo, wakati wa uwasilishaji wa fatwa hiyo jana Ijumaa.

Amesema mapambano ya silaha dhidi ya Israel ni wajibu wa kidini kwa Waislamu wote wenye uwezo, na kuzitaka serikali za Kiislamu kuchukua hatua za haraka kukomesha "mauaji ya kimbari" ya Wapalestina.

Mbali na operesheni za kijeshi, wanazuoni hao wametoa wito wa kuwekewa mzingiro Israel kuanzia nchi kavu, baharini na angani, ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa njia kuu za majini na angani zinazodhibitiwa na Waislamu, zinazoelekea au zinazohusishwa na Israel.

Wanazuoni wa Kiislamu watoa fatwa; Mataifa ya Kiislamu yaunge mkono Muqawama wa Palestina

Kadhalika fatwa hiyo inapiga marufuku usambazaji wa mafuta, gesi, au rasilimali yoyote kwa Israel, ambayo inaweza kusaidia kampeni yake ya mauaji ya halaiki huko Gaza. "Imeharamishwa kumuunga mkono adui kafiri (Israel) katika kuwaangamiza Waislamu huko Gaza, pasi na kujali aina ya uungwaji mkono," Qaradaghi amebainisha.

Aidha fatwa hiyo inazitaka jumuiya za Kiislamu nchini Marekani kuushinikiza utawala wa Donald Trump kuchukua hatua madhubuti za kukomesha uvamizi wa Israel na kushinikiza amani.

Maulamaa hao wa Kiislamu wamesisitiza kuwa, ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza hauwezi kuvumiliwa; na jamii ya kimataifa lazima ichukue hatua haraka ili kukomesha mauaji ya kimbari ya Kizayuni katika eneo hilo.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha