11 Aprili 2025 - 22:56
Hatua Tano na Muhimu Kabla ya Kuingia Katika Mjadala au Kabla ya Kufanya Mjadala na Mtu yeyote | Bila hatua hizi huo sio Mjadala Bali ni Kupoteza Muda

Kabla hujafanya mjadala wowote na mtu yeyote, unapaswa kuzingatia nukta za kimjadala na muhimu ili uepuke mapema kupoteza muda wako kwa kuingia katika mjadala usiokuwa na matunda yoyote.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA - Samahat Sheikh Abdughani Al-Khatib amebainisha nukta muhimu zinazotakiwa kwa yeyote mwenye kudhamiria kufanya mjadala na mtu yeyote yule.

Kwamba kabla hujafanya mjadala wowote, unapaswa kuzingatia nukta hizo za kimjadala na muhimu ili uepuke mapema kupoteza muda wako kwa kuingia katika mjadala usiokuwa na matunda yoyote.

Amesema: Unapotaka kuingia katika mjadala wowote fuata hatua hizi zifuatazo:

🔹Hatua ya kwanza: Lazima ujue lengo la huo mjadala, kwamba je, kile mnachotaka kukijadili kinastahiki kujadiliwa na kuchukua muda wenu wa thamani au la?. 

Ikiwa utagundua na kutambua kuwa hicho mnachotaka kukijadili,  kinastahiki kujadiliwa, ndio uje katika hatua ya pili.

🔹Hatua ya pili: Je, kitu hicho kina manufaa gani katika Umma na jamii?.

🔹Hatua ya tatu: Kila mmoja awe muaminifu na nafsi yake ya kuwa yupo katika kuitafuta haki na siyo kuonyesha mbawa zake.

Hakikisha Haki unayoitafuta ni Haki kweli kweli, na mbio zako zipo katika kuitetea Haki hiyo, au kuipigania Haki hiyo, kwani mijadala mingi haina natija kwa vile kila mmoja anataka kudhihirisha ushindi hata ikiwa ni kwa matusi na ngumi (ili mradi tu ashinde hata kama anachokifanya ni batili)..

🔹Hatua ya nne: Kuweka wazi kadhia mnayotaka kuijadili (lazima iwe ni mada Maalum ili kuepuka kuongelea kadhia Mia ndani ya kitu kimoja), kwa sababu bila kuweka wazi mada husika ikajulikana, mtaishia kupoteza muda wenu wa thamani pasina tija yoyote.

🔹Hatua ya Tano: Mkubaliane marejeo mtakayo yategemea katika kuthibitisha kile mnachokipigania na kukijadili, mnatumia Vyanzo vipi?! Lazima vyanzo hivyo viwe vinakubalika pande zote mbili, mfano:

Kuleta kwenye mjadala Hadithi ambayo ni Sahihi kwa pande zote mbili zinazojadiliana, sio upande huu ulete Hadithi ambayo kwa mletaji yeye anaona kwake ni Hadithi, lakini kwa upande mwingine ni Hadithi feki na batili, hivyo lazima mzingatie kuleta Hadithi zinazokubalika Usahihi wake kwa pande zote mbili, yaani upande huu unaiona ni Hadithi Sahihi, na upande wa pili unaikubali pia kuwa ni Hadithi Sahihi, lazima mhakikishe Vyanzo vyenu vinakubalika na kuainisha vyanzo hivyo, kwani bila kufanya hivyo kila mmoja atasema atakalo yeye kwa upande wake,  pasina kuchunga adabu za hiwaru / mjadala wa pande mbili.

Hatua hizi zikifuatwa vizuri, ni vyema kuingia katika mjadala na mjadala huo utakuwa ni mjadala Mzuri wenye natija nzuri. Tofauti na hilo, jitoe au usifanye mjadala usiokuwa na nukta hizo zilizotajwa hapo juu, maana utakuwa unapoteza muda wako wa thamani kushiriki mjadala usiokuwa na Mantiki yoyote.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha