12 Mei 2015 - 17:58
 Maandamano ya kumpinga rais yaendelea Burundi

Polisi nchini Burundi wamefyatua risasi kwa waandamanaji leo wakati rais Pierre Nkurunziza akikaidi mbinyo wa kimataifa kuacha juhudi zake za kuwania urais kwa kipindi cha tatu, kabla ya mkutano wa kikanda kuzungumzia mzozo huo.

Mtu  mmoja  ameuwawa  katika  ghasia  hizo  mpya  na  polisi  katika mitaa  ya  mji  mkuu  wa  Burundi, Bujumbura , wakati  watu  wengine wawili  wameripotiwa  kuuwawa  usiku  katika  mripuko  wa  guruneti.

Idadi  ya  vifo  sasa imefikia  watu  20  waliouwawa  katika  wiki zaidi  ya  mbili  za  maandamano  dhidi  ya  serikali na  yanakuja wakati  viongozi  wa  mataifa  ya  Afrika  mashariki  wanajitayarisha kwa  mkutano  wa  dharura  nchini  tanzania  kesho.

Zaidi  wa  Waburundi  50,000  wameikimbia  nchi  hiyo  wakikimbialia katika  nchi  jirani  tangu ghasia  hizo  kuanza.

Rais Joseph Kabila  wa  jamhuri  ya  kidemokrasi  ya  Congo, makamu  wa  rais  wa  Afrika  kusini Cyril Ramaphosa  na mwanadiplomasia  wa  ngazi  ya  juu  wa  Marekani  kwa  ajili  ya Afrika  Linda Thomas-Greenfield  pia  wanatarajiwa  kuhudhuria mkutano  huo.