31 Oktoba 2015 - 19:42
 Milipuko ya mabomu yatokea visiwani Zanzibar

Milipuko miwili midogo imetokea leo katika barabara za visiwani Zanzibar lakini haikusababisha maafa yoyote.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Milipuko miwili midogo imetokea leo katika barabara za visiwani Zanzibar lakini haikusababisha maafa yoyote. Milipuko hiyo imetokea karibu na njia panda yenye shughuli nyingi katika mji wa Zanzibar, hali iliyosababisha watu kukimbilia usalama wao. Zanzibar imeshuhudia vurugu za  kidini na kisiasa katika miaka ya karibuni -- ikiwa ni pamoja na milipuko ya maguruneti -- huku vurugu hizo zikiathiri sekta muhimu ya utalii visiwani humo. Jana jioni, watalaamu wa mabomu walitegua bomu katikati mwa Mji Mkongwe. Tume ya uchaguzi visiwani humo ZEC ilifuta uchaguzi wa Jumapili iliyopita, kutokana na dosari. Mgombea wa chama cha upinzani CUF Seif Sharif Hamad aliyejitangaza mwenyewe kuwa ni mshindi wa uchaguzi huo,  hapo jana ametishia kuwaachilia na kuwashawishi wananchi kudai haki yao kwa amani ikiwa hali hiyo haitatatuliwa ifikapo Jumatatu akisema hatokubali kushindwa na mpinzani wake mkuu, rais wa sasa Ali Mohamed Shein wa Chama Cha Mapinduzi - CCM.

Mwisho wa habari/ 291