Shirila la habari la ABNA linaripoti kuwa: Baada ya Uturuki kujiingiza kwenye shimo refu kwa kuidungua denge ya kivita ya Urusi iliyokuwa katika mipaka ya Syria ikiwashambulia magaidi na kupelekea uhusiano wa nchi hiyo na Urusi kuharibika kabisa, hatimaye Uturuki nayo yajitutumua na kutishia kuiwekea vikwazo Urusi.
Vita vya maneno kati ya Uturuki na Urusi vinazidi kushika kasi, baada ya Uturuki kujitutumua na kuelezea uwezekano wa kuchukua hatua dhidi ya Urusi na kusema kwamba itaweka vikwazo iwapo itahitajika kufanya hivyo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu wakati akizungumza bungeni na wabunge wa chama chake kinachotawala cha AK. Hata hivyo, ameongeza kusema nchi yake itaendelea kuacha milango wazi kwa ajili ya mazungumzo na Urusi.
Urusi imeweka vikwazo kadhaa vya kiuchumi dhidi ya Uturuki, baada ya Uturuki kuidungua ndege ya kivita ya Urusi karibu na mpaka na Syria na Uturuki, mwezi uliopita, kutokana na Uturuki kudai kuwa ndege hiyo ilipuuza onyo lililotolewa mara kadhaa la ndege hiyo kuvuka mpaka na kuingia katika anga yake.
Hata hivyo, Urusi ambayo imeyakanusha madai hayo, imelijibu shambulizi la Uturuki kwa kupeleka mfumo wa kuweka ulinzi angani kukinga makombora ya masafa marefu katika kambi yake nchini Syria.
Aidha, Davutoglu amesema anataka kuzuru Iraq, haraka iwezekanavyo kujaribu kutuliza mzozo kuhusu hatua ya Uturuki kuwapeleka wanajeshi wake nchini Iraq bila ya idhini ya Iraq kwa madai kwamba ina nia ya kuwapatia mafunzo baadhi ya wapiganaji wa Iraq katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh ambalo linasadikiwa kuwa na mafungamano ya biashara za mafuta na Uturuki.
Davutoglu amwandikia barua mwenzake wa Iraq
''Nimemwandikia barua Waziri Mkuu wa Iraq, Haidar Abadi. Nina matumaini Waziri wa Ulinzi wa Iraq atazuru Uturuki hivi karibuni na mimi nitazuru Baghdad kwa ajili ya mkutano wa ngazi ya juu utakaozungumzia mashauriano. Nataka kuwaeleza watu wa Iraq kwamba siku zote tutawasaidia kupambana na ugaidi. Wairaqi wote ni ndugu zetu,'' alifafanua Davutoglu.
Serikali ya Iraq imetoa masaa 48 kwa Uturuki itoe majeshi yake la sivyo Iraq itachukua hatua kali.
Uturuki imetangaza kusitisha kupeleka wanajeshi wake kaskazini mwa Iraq kwa sasa, lakini haitawaondoa wanajeshi ambao tayari wako huko na imedai kuwa wanajeshi hao ni sehemu ya kikosi cha kuwapatia mafunzo na kuwapa vifaa wanajeshi wa Iraq.
Serikali ya Iraq imesema haijawahi kukialika kikosi kama hicho na italiwasilisha suala hilo katika Umoja wa Mataifa, iwapo hawatoondolewa. Davutoglu amesema zaidi ya watu 2,000 wamepatiwa mafunzo katika kambi hiyo ya kaskazini mwa Iraq.
Ama kwa upande mwingine Uturuki imesisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa ''maeneo salama'' kaskazini mwa Syria na kutekeleza haraka mapendekezo ya kutoa mafunzo na kuwapatia vifaa magaidi wenye msimamo wa wastani ili kuendeleza jinai nchini Syria.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, wakati akizungumza na maafisa kutoka maeneo ya jirani kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Ankara.
Wakati huo huo, mwanadiplomasia mmoja katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, amesema Urusi ina mpango wa kuzungumzia vitendo vya kijeshi vinavyofanywa na Uturuki nchini Syria na Iraq, katika mkutano wa baraza hilo.
Uturuki ambayo ilidungua ndege ya Urusi kwa madai ya kuingia kwenye anga la Uturuki kwa sekunde kadhaa, leo hii inatuma majeshi na kuingia ardhi ya Iraq bila ya idhini ya nchi hiyo, na kudai kuwa inakwenda kuwapa mafunzo wanajeshi wa Iraq.
Weledi wa mambo wanasema kuwa Uturuki inalengo la kutafuta njia mpya ya kusafirisha mafuta ya wizi inayouziwa na kundi la kigaidi la Daesh, baada ya njia za mwanzo kufungwa na majeshi ya Urusi na kusababisha hasara kubwa kwa Uturuki na washirika wake.
Mwisho wa habari/ 291