31 Januari 2016 - 19:19
Majeshi ya Tanzania yaanza kuwasaka  majangili

Jeshi la Serikali ya Tanzania limeanzisha msako maalumu kwa ajili ya kuwatia mbaroni majangili wanaoua wanyama pori kiholela

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Jeshi la  Serikali ya Tanzania limeanzisha msako maalumu kwa ajili ya kuwatia mbaroni majangili  wanaoua wanyama pori kiholela, hususan wale waliohusika na kuidungua helicopter na kumuua rubani wake raia wa Uingereza wakati  wa operesheni ya kuwasaka majangili wanaohusika kuwaua tembo katika hifadhi za taifa nchini humo. Dan Friedkin ambaye ni mwenyekiti wa taasisi ya uhifadhi wanyamapori ya Friedkin Conservation Fund  alithibitisha kuuawa kwa rubani huyo   wa kiingereza  Roger Gower aliyekuwa akiwasaka wawindaji hao haramu kwa kutumia Helcopter hiyo kabla ya kudunguliwa kutoka ardhini  na silaha iliyotambulika kuwa ni ya aina ya AK-47  ijumaa wiki hii katika hifadhi ya wanyamapori ya  Maswa nchini humo. Waziri wa maliasili na utalii nchini Tanzania Professa Jumanne Maghembe amethibitisha taarifa hizo. Operesheni ya kuwasaka majangili hao inaendeshwa kwa ushirikiano wa taasisi ya Friedkin Conservation Fund na serikali ya Tanzania ili kudhibiti uwindaji haramu ambao  katika siku za hivi karibuni unaonekana kuongezeka kwa kiwango cha juu nchini humo.  Kwa mujibu wa Sensa iliyofanywa mwezi Juni mwaka jana idadi ya tembo nchini humo imepungua kutoka 110,000 kwa mwaka 2009 hadi tembo 43,000 mwaka 2014.

Mwisho wa habari/ 291