Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Mapigano makali yamesitishwa kwa muda nchini nchini Syria halikadhalika mashambulizi ya anga ya Urusi wakati usitishaji wa uhasama ukianza kutekelezwa kwa siku ya kwanza Jumamosi leo tarehe 27 mwezi wa 2 mwaka 2016.
Chini ya makubaliano kati ya Marekani na Urusi yaliyokubaliwa na serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria na maadui zake wengi, mapigano yanapaswa kusitishwa ili kutowa nafasi kwa misaada kufikishwa kwa raia na ili mazungumzo yaanze ya kukomesha vita vya nchi hiyo ambavyo vimeuwa zaidi ya watu 250,000 na kuwapotezea makazi wengine milioni 11.
Urusi imesema inakusudia kuendelea kufanya mashambulizi katika maeneo yanayoshikiliwa na wapiganaji wa makundi ya kigaidi ambao hawahusiki na suluhu hiyo lakini imesema itasitisha safari zake zote juu ya anga ya Syria katika siku ya kwanza ya suluhu hiyo ili kuhakikisha hakuna makosa katika shabaha zake za mashambulizi.
Waasi wanaoungwa mkono na Marekani na Saudia arabia wamedai kuwepo kwa ukiukaji wa suluhu wa mara kwa mara unaofanywa na serikali na kamanda mmoja ameonya kwamba iwapo ukiukaji huo hautokaguliwa unaweza kupelekea kusambaratika kwa makubaliano hayo.
Vyombo vya habari vya taifa vimeelezea kuwepo kwa mashambulizi ya roketi karibu na Damascus yaliofanywa na kundi la kigaidi la Daesh ambalo pia linadhaminiwa na Saudia arabia, Uturuki, Marekani na washirika wao. Lakini kwa jumla kiwango cha mashambulizi ya majeshi ya serikali dhidi ya magaidi wanaoungwa mkono na Marekani kimepunguwa sana.
Matumaini ya amani
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Staffan de Mastura amesema katika mkutano na waandishi wa habari usiku wa manane mjini Geneva kwamba " Tuombe makubaliano hayo yataweza kufanya kazi kwa sababu kusema kweli hii ni fursa bora kabisa ambayo wanaweza kufikiria watu wa Syria wameweza kuwa nayo katika kipindi cha miaka mitano iliopita,kuona kitu fulani kizuri na kutaraji kitahusiana na amani."
Amesema anatarajia kutakuwepo na ukiukaji wa makubaliano hayo mara kwa mara lakini ametowa wito kwa wahusika kuchukuwa hatua za kujizuwia na kudhibiti kupamba moto kwa mzozo huo unaochochewa na Marekani na washirika wake kwa lengo la kumuondoa madarakani rais Bashar asad.
Makubaliano hayo ni ya kwanza ya aina yake kujaribiwa katika kipindi cha miaka minne na iwapo yataweza kufanya kazi yatakuwa makubaliano yenye mafanikio makubwa kabisa ya suluhu kuwahi kushuhudiwa hadi sasa katika vita hivyo vya miaka mitano.
Makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani
Makubaliano hayo hayajumuishi makundi yenye nguvu ya wapiganaji wa kigaidi wanaodhaminiwa na Marekani na washirika wake kama vile kundi la kigaidi la Daesh na Nusra Front ambalo ni tawi la Al Qaeda nchini Syria. Kundi la kigaidi la Daesh limedai kuhusika na shambulio la kujitolea muhanga la mripuko wa gari katika jimbo la Hama. Kundi la Nusra limetowa wito wa kuongezwa mashambulizi maradufu.
Urusi na serikali ya Syria zinasema zitaendelea kupambana na makundi hayo ya kigaidi na waasi wengine wanaodhaminiwa na Marekani, nakusema wana hofu wanaweza kutumia kisingizio hicho kuwashambuia wao.
Usitishaji huu wa mapigano ni hitimisho la juhudi za kidiplomasia ambazo zimezingatia kubadilika kwa medani ya mapambano tokea Urusi na Iran zijiunge katika vita hivyo hapo mwezi wa Septemba kwa mashambuzi ya anga kumsaidia Assad. Kuingilia kwa Urusi na Iran kumefuta kabisa matumaini ya Marekani na waliokuwa nayo maadui zake Assad kwa miaka mitano yakishajiishwa na mataifa ya Kiarabu na yale ya magharibi ya kumn'gowa kwa kutumia nguvu.
Vikosi vya serikali vikisaidiwa na mashambulizi ya anga ya Urusi na vikosi vya ardhi vikiongozwa na wataalamu wa vita kutoka Iran vimesonga mbele katika wiki za hivi karibuni na kuukaribia mji wa Allepo ambao ndio uliokuwa ngome kubwa kabisa ya magaidi wanaoungwa mkono na Marekani nchini Syria.
Marekani imesema wakati umefika kwa Urusi kuonyesha kwamba iko makini kuhusu usitishaji wa mapigano kwa kuheshimu ahadi zake za kutoshambulia makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani nchini Syria.
Makubaliano haya yanaashiria kuwa Marekani na washirika wake wanaodhamini magaidi wamenyoosha mikono na kukubali kufanya sulhu na serikali halali ya Syria inayoungwa mkono na Urusi na Iran.
Mwisho wa habari/ 291