24 Novemba 2020 - 11:20
Mazungumzo baina ya makundi hasimu ya Libya yanaendelea

Makundi hasimu ya Libya yanaendelea na awamu ya pili ya mazungumzo yao yalilyoanza jana Jumatatu kujadiliana njia za kiutaalamu za kuunda serikali ya mpito ambayo itaongoza hadi utakapofanyika uchaguzi mkuu mwezi Disemba 2021.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mjumbe maalumu wa hivi sasa wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya, Stephanie Williams, ndiye aliyeongoza mazungumzo hayo ya jana Jumatatu yaliyofanyika kwa njia ya Intaneti baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo hayo huko Tunisia kushindwa kutangaza mamlaka ya kusimamia mchakato wa kuunda serikali hiyo ya mpito.

Mazungumzo hayo yanayowashirikisha wajumbe 75 wa makundi mbalimbali hasimu ya Libya yalifikia makubaliano ya kufanyika uchaguzi wa Rais na Bunge, tarehe 24 Disemba 2021. Wajumbe hao walikubaliana pia kuunda kamati ya kujitolea ya wanasheria ambayo itaandaa kalibu na fremu ya sheria za uchaguzi.

Jukwaa hilo la kisiasa ndizo juhudi za karibuni kabisa za kimataifa za kukomesha machafuko ya miaka mingi katika nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika ambayo ina utajiri mkubwa wa mafuta. Libya haijawahi kuwa na utulivu wa angalau siku moja tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni ya kumng'oa madarakani Kanali Muammar Gaddafi, machafuko ambayo yaliishia kuuawa kiongozi huyo wa zamani wa Libya.

Huku hayo yakiripotiwa, jana mbunge mmoja wa Libya alinukuliwa akisema kuwa, wabunge wa nchi hiyo wanajiandaa kuanza mazungumzo kwa ajili ya kuyaunganisha mabunge mawili ya nchi hiyo yenye makao yao mashariki na magharibi mwa Libya. Mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema, wabunge wa mabunge hayo yenye makao yao katika miji ya Tobruk na Tripoli  wanajiandaa kushiriki kikao maalumu cha kujadili suala hilo katika mji wa bandari wa Tangier nchini Morocco.

342/