Shirika la Habari la Kimataifa Ahlul-Bayt (as) -ABNA-: Qur’an imemsifu na pia kumlaumu binadamu. Sifa za juu kabisa na lawama kubwa zaidi katika Qur’ani zimeelekezwa kwa binadamu; imemfanya kuwa bora kuliko mbingu na ardhi na hata malaika, na wakati huohuo imemweka chini kuliko majini na wanyama. Kwa mtazamo wa Qur’ani, binadamu ni kiumbe mwenye uwezo wa kuutawala ulimwengu na kuwatumikisha malaika, na pia anaweza kushuka hadi kwenye “asfal al-safilin” (chini kabisa). Ni juu ya binadamu mwenyewe kuamua kuhusu nafsi yake na kuamua hatima yake ya mwisho.
Qur’ani katika asili ya kila binadamu, hata kama ni Firauni, inamtambua binadamu wa kweli, na kwa hiyo Mitume wa Mwenyezi Mungu wanapokuja kupambana na Firauni, jambo la kwanza wanalojaribu ni kuamsha ule ubinadamu wa ndani ulio ndani yake umpinge yeye mwenyewe. Ana fitra inayomfahamu Mwenyezi Mungu; ana ufahamu wa Mungu wake katika kina cha dhamiri yake. Ukanushaji na mashaka yote ni maradhi na upotovu kutoka kwenye asili halisi ya binadamu.
Katika asili ya Binadamu: Ana heshima na utukufu wa kimaumbile; Mwenyezi Mungu amemfanya bora juu ya viumbe vingi vyake. Anapojitambua kweli, anahisi na kufahamu heshima na utukufu huo, na kujiona yuko juu kuliko unyonge, uchafu, utumwa na tamaa mbaya:
“Kwa hakika Tumewatukuza wanaadamu na Tumevibeba katika nchi kavu na baharini, na Tumewapa vyakula vizuri na Tumevifanya viumbe vingi Tulivyoviumba kuwa bora kwao.” [1]
Ana dhamiri ya kimaadili: kwa amri ya ilhamu ya fitra, anatambua baya na zuri:
“Naapa kwa nafsi ya mwanaadamu na kwa aliyemuumba kwa uwiano, kisha akamfunulia uovu na wema wake.” [2]
Imam Khomeini anaeleza kuwa Qur’ani Tukufu inaitambulisha fitra ya binadamu kama fitra ya Kimungu; fitra ya binadamu imeumbwa kwa mkono wa nguvu ya Haki Aliyetukuka na imetoka katika ulimwengu wa usafi na utakatifu, hivyo mradi tu fitra yake ya asili haijatiwa uchafu, hubakia na nuru na usafi wa ndani na hutafuta ukamilifu kamili na kheri, huku akikimbia shari. [3]
Kwa mtazamo wake, mradi binadamu anabaki kwenye fitra yake ya Kimungu, huwa katika hali njema zaidi ya kimaumbile, kwani ameumbwa juu ya umbo bora zaidi (ahsani taqwim), na akipotoka kutoka kwenye njia ya fitra, anaweza kushuka hadi kwenye daraja la mwisho la maangamizi. [4]
Ana haiba huru na ya kujitegemea, ni mlinzi wa amana ya Mungu, ana risala na jukumu, ameombwa kwa juhudi na ubunifu wake kuistawisha ardhi na kwa hiari yake kuchagua moja ya njia mbili: ya ufanisi au ya upotevu.
“Hakika Sisi tuliwapa mbingu na ardhi na milima amana, zikakataa kuibeba na zikaogopa, lakini mwanaadamu akaibeba. Hakika yeye ni dhalimu na mjinga.” [5]
“Hakika Sisi Tumemuumba mwanaadamu kutokana na tone la manii lililochanganywa, ili Tumjaribu, na Tukamfanya asikie na aone. Hakika Tumemuonesha njia, akitaka atakuwa mwenye shukrani au akitaka atakufuru.” [6]
Marejeo:
1. Al-Isra/17:70
2. Ash-Shams/91:8-9
3. Khomeini, Ruhullah, Sharh-e Hadith Junud-e Aql wa Jahl, uk. 113-115, Tehran, Taasisi ya Kudhibiti na Kuchapisha Kazi za Imam Khomeini, 1382.
4. Khomeini, Ruhullah, Taqrirat-e Falsafe-ye Imam Khomeini, j. 3, uk. 114, Tehran, Taasisi ya Kudhibiti na Kuchapisha Kazi za Imam Khomeini, 1385.
5. Al-Ahzab/33:72
6. Ad-Dahr/76:2-3
Your Comment