Hamas imezitaja hatua hizo kuwa zinadhihirisha msimamo imara dhidi ya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Harakati ya Hamas imesema kuwa inakaribisha pakubwa misimamo ya Uturuki katika kuwaunga mkono watu wa Palestina kutokana na kuendelea vita vya mauaji ya kimbari ya adui Mzayuni, mtenda jinai.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina yenye makao yake huko Gaza pia imezitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu kuchukua hatua sawa na Uturuki dhidi ya utawala wa Israel ili kuhitimisha mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza ambako Wapalestina zaidi ya 63,000 wameuliwa shahidi.
Hakan Fidan Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki alisema jana Ijumaa katika kikao cha dharura cha Bunge la nchi hiyo kuhusu Gaza kwamba nchi yake imekata kabisa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na Israel na imefunga anga na bandari zake kwa ndege na meli za Israel kutokana na vita vya mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala huo huko Gaza.
"Tumekata mahusiano yetu yote ya kibiashara na Israel. Haturuhusu meli za Uturuki kuelekea katika bandari za Israel. Vilevile haturuhusu ndege zao kuingia katika anga yetu," alisema jana Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki.
Katika taarifa yake nyingine ya jana Ijumaa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) iliunga mkono wito wa Malasysia wa kutaka Israel ifukuzwe katika Umoja wa Mataifa kutokana na mauaji ya kimbari inayofanya katika Ukanda wa Gaza.
Your Comment